Na Gladness Mboma
BARA la Afrika limepewa changamoto ya kujenga uwezo wa kutambua rasilimali walizonazo na kushirikiana na wataalam wa kimataifa kunufaisha wananchi wake na kuepusha migogoro.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa Kimataifa (UNDP),Bw.Alberic Kacou, wakati alipomtembelea ofisini kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Bw. Regnald Mengi.
Alisema kuwa ni vema kila nchi ikachukua hatua ya kuzuia migogoro kwa kueleza mambo kwa uwazi ili kuepusha manung'uniko ambayo usababisha chuki na maafa.
"Rasilimali za nchi lazima ziwe na baraka badala ya laana kwa Taifa husika, maandalizi ya matumizi na mgawanyiko mzuri wa rasilimali katika elimu afya...kutaepusha upelekwaji wa majeshi ya Umoja wa Mataifa kuzuia ghasia,"alisema.
Alisema Umoja wa Mataifa huwa hauna jeshi lake, ila nchi wanachama ndio uombwa kupeleka majeshi kutuliza ghasia na jambo hilo ufanyika kwa kuchelewa.
Akizungumzia suala la nishati nchini, alisema Tanzania ni lazima itoe kipaumbele katika kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana kwa bei nafuu ili wananchi waweze kuimudu.
Bw. Kacou alisema sekta ambazo zinatokana na umeme kama miundombinu uboreshaji wa huduma za jamii zipewe kipaumbele.
Alisema Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi kama mbuga za wanyama na iko katika nafasi nzuri ya kutoka katika hali ya kiuchumi iliyopo sasa na kuingia katika maisha bora kwa wananchi wake.
Naye Bw. Mengi alisema kuna umuhimu wa Tanzania kutumia wataalam wake ipasavyo kuendesha kwa faida miradi mikubwa mfano madini.
"Na si vema kusubiri mgeni kuja kuonyesha mahali yalipo madini, mafuta na hatimaye kusubiri mgeni achimbe na kuwapa kidogo,"alisema..
Bw. Mengi alimuuliza, Bw.Kacou kama kuna uwezekano wa kuwepo mfuko maalum wa kusaidia walemavu na kutaka Umoja wa Mataifa kuwezesha walemavu kujimudu kiuchumi.
Akijibu hoja hiyo, Bw. Kacou alisema Umoja wa Mataifa una mpango wa kuendeleza utaratibu wa kutoa mafunzo ya kiufundi kwa walemavu ili kuwapa uweledi na kuweza kupata ajira au kujiajiri wenyewe.
No comments:
Post a Comment