28 March 2012

Ligi ya Taifa kuanza Aprili 22

Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imepitisha michuano ya Ligi ya Taifa Ngazi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa ianze Aprili 22, mwaka huu kwenye vituo vitatu tofauti.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema juzi ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa vyama vya mikoa kuwasilisha TFF majina ya mabingwa wao, ambapo ni mikoa minne tu iliyomudu kufanya hivyo kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF.

Aliitaja mikoa hiyo na mbingwa wake katika mabano kuwa ni Kigoma (Kanembwa FC ya Kibondo), Ruvuma (Mighty Elephant ya Songea), Kilimanjaro (Forest FC ya Siha) na Dodoma (CDA ya Dodoma Mjini).

Alisema kutokana na hali hiyo, kamati imeongeza muda hadi Aprili 9, mwaka huu kwa mikoa ambayo haijawasilisha majina ya mabingwa wao iwe imefanya hivyo kwa watakaochelewa hawatapata fursa ya kucheza ligi hiyo.

Mbali na hilo, kamati hiyo imepanga makundi matatu ya ligi hiyo ambapo Kundi A lina mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Lindi na Mtwara.

Alisema Kundi B lina mabingwa wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Singida na Dodoma na Kundi C ni Dar 1, Dar 2, Dar 3, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Aliongeza kuwa TFF inakaribisha maombi ya uenyeji kwa kila kundi na taarifa rasmi itatumwa kwa vyama vya mikoa kueleza masharti ya kutimiza kabla ya mkoa kupewa kituo cha ligi hiyo.

Alisema mshindi katika kila kundi na washindwa bora (best losers), wawili kutoka kwenye makundi yenye timu nane watapanda daraja msimu ujao kucheza Ligi Daraja la Kwanza.

Wambura alisema pia timu zinatakiwa ziwe zimefanya usajili wa wachezaji kufikia Aprili 10, mwaka huu wakati Aprili 11 mpaka 18 itakuwa ni kipindi cha kutangaza majina na pingamizi.

No comments:

Post a Comment