27 March 2012

CCM waisihi NEC iwalinde Arumeru

*Wadai vyama pinzani vimeanza mchezo mchafu
*Mbowe amvaa RC, adai CCM inakaribia kufa
Pamela Mollel na Queen Lema, Arumeru
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwachukulia hatua za kisheria wanachama na viongozi wa vyama pinzani kwa madai ya kumdhalilisha mgombea anaewakilisha chama hicho katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, Bw. Sioi Sumari.

Mbunge wa Simanjiro, mkoani Manyara, Bw.Christopher Ole Sendeka, aliyasema hayo jana wakati akimnadi Bw. Sumari katika Kata ya Nkoanrua, wilayani hapa.

Alisema wafuasi wa vyama pinzani jimboni humo wamechana picha za Bw. Sumari, zingine kupakwa rangi mdomoni 'lipstik', kuzichora hereni katika masikio na kuzibandika mitaani huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na taratibu ya uchaguzi.

“Watu wanaofanya hivi wanaeleweka na wamedhamiria, wanafahamu kuwa kanuni za uchaguzi zinazuia matendo yasiyofaa kama haya hivyo naiomba NEC ichukue hatua kali.

“Mambo haya yanaweza kusababisha machafuko kwenye kampeni kwani wafuasi wa CCM hawatavumilia matendo haya,” alisema.

Wakati huo huo, diwani wa Kata ya Ndoombo Nkorisambu, Bw. Wilson Nyiti, amevitaka vyama vya upinzani kutekeleza kwa vitendo miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema viongozi wa vyama hivyo wanawadanganya wananchi kuwa Serikali ya CCM haijawaletea maendeleo katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru

“Ni vyema wapinzani wakatambua na kuthamini maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya CCM badala ya kupotosha ukweli kwa mfano, kata hii miaka ya nyuma baarabara zilikuwa hazipitiki lakini kutokana na juhudi za Serikali, miundombinu imeboreshwa,” alisema Bw. Nyiti.

Kwa upande wake, Bw. Sumari aliwataka wakazi wa kata hiyo kuwapuuza wapinzani na kumchagua yeye awe mwakilishi wao bungeni ili aendeleza mikakati ya maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa na marehemu baba yake, Bw. Jeremiah Sumari.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, amesema Serikali ya CCM inakaribia kufa kwa sababu ya kutegemea zaidi rushwa na nguvu ya dola.

Bw. Mbowe aliyasema hayo jana wakati akimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho Bw. Joshua Nassari, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Maruvango, kilichopo Kata ya Leguruki.

Alisema CCM imekuwa ikijionesha hadharani jinsi wanavyotumia mabavu hata katika masuala ambayo hayahitaji kutumia nguvu.

“Kuna kila dalili za chama tawala kufa kutokana na mambo wanayofanya, hii ni faraja kwetu, sisi tutaendelea kusonga mbele hakuna kurudi nyuma,” alisema Bw. Mbowe.

Aliongeza kuwa, kitendo cha mfuasi wa CCM aliyemtaja kwa jina la Bw. Elibariki Kaleria, kumpiga mfuasi wa CHADEMA Bw. Elia Samweli Nnko (65), kwa sababu ya kuhama chama hicho ni uonevu.

Bw. Mbowe alimvaa Mkuu wa Mkoa huo Bw. Magesa Mulongo na kudai hajui majukumu yake kwa sababu ya kuacha ofisi badala yake amekimbilia Kata ya Kingori kumnadi mgombea ubunge wa CCM.

“Namsihi Bw. Mulongo aache kutumia kofia aliyonayo vibaya, achague moja kama ni siasa au Ukuu wa Mkoa ili atumikie wannchi akiwa ofisini kwake,” alisema Bw. Mbowe.

3 comments:

  1. NEC IWALINDE CCM KWA KUWA WAMEWAPIGA BAADHI YA WAZEE NA WANACHAMA WA CHADEMA HATA KUWAUMIZA SEHEMU ZA SIRI? KAMA NI KULINDANA NDIO HUKO.

    ReplyDelete
  2. Ofcourse NEC Inailinda ccm,polisi wanailinda ccm,usalalma wanailinda ccm.Lakini wakiwaachia wananchi wachague wanaemtaka watachagua tu chadema.We si utaona.Eti Tanzania kuna Demokrasia nani kakwambia.CCM wanafanya kila njia za wizi wa kula,rushwa,angalia sioi au kuoa alivyopita,kulikuwa ni rushwa tupu hata ccm wenyewe wamekiri.Hivyo ndo sitahili ya ccm.Lakini safari hii na nyinginezo chadema juuuuuuuuuuu.

    ReplyDelete
  3. HONGERA CHADEMA KUUKWA UBUNGE ARUMERU

    ReplyDelete