23 March 2012

Kikwete adhibiti posho za wabunge

                           Rais Jakaya kikwete
*Ni baada ya kilio cha wananchi,wastaafu
*Ni kile cha kupinga nyongeza za posho zao
Na Grace Ndossa
HATIMAYE dawa ya wabunge na watumishi wengine wa umma kujipangia mishahara na marupurupu makubwa kiasi cha kulalamikiwa na wananchi, imepatikana baada ya Rais Jakaya Kiwete, kuunda Bodi ya Mishahara na Marupurupu katika Utumishi wa Umma.

Rais Kikwete ameunda bodi hiyo huku ndani ya jamii kukiwa na mvutano mkubwa wa kupinga wabunge kujiongezea posho kutoka sh. 70,000 kwa siku hadi sh. 200,000 kwa kile kilichoelezwa na Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda kwamba ni kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilieleza kuwa bodi hiyo itakuwa ni kwa ajili ya mishahara na marupurupu katika utumishi wa umma.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu Utumishi Bw. George Yambesi, ilieleza kuwa uteuzi wa bodi hiyo ulianza tangu Februari 20, mwaka huu.

"Rais Kikwete ameunda Bodi ya Mishahara na Marupurupu katika Utumishi wa Umma na kumteua mwenyekiti wa bodi hiyo kuwa Bw. Vicenti Mrisho," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa  Katibu Mkuu wa bodi hiyo ni Bi Tamika Mwakahesya wajumbe ni Bi. Assumpta Ndimbo, Bi Celina Wambura, Balozi Charles Mutalemwa, Bw.Yahya Mbila, Bw. Hussein Seif na Bw.Arthur Mwakapugi.

***Wachambuzi wa mambo

Wachambuzi wa mambo wanasema kuanzishwa kwa bodi hiyo kutasaidia kuweka uwiano sawa wa marupurupu na mishahara kwa watumishi wa umma, hivyo kuondoa malumbano kama yaliyotokea wakati Spika wa Bunge, Bi. Makinda alipothibitisha posho za wabunge kupanda kutoka sh. 70,000 hadi 200,000.

Pia baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani walisimama imara kupinga nyongeza ya posho hizo, hatua iliyoonesha kuwagawa wabunge.

***Msimamo wa Sumaye

Hatua hiyo pia ilimfanya Waziri Mkuu Mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, kuongelea suala na kukaririwa na vyombo vya habari akipinga posho hizo.

Alionya kuwa nyongeza za posho zisizofuata utaratibu kwa watumishi wa umma ni hatari na ni utawala mbaya kwa nchi.

Alisema suala la posho ni jambo ambalo sasa limekuwa tatizo kwa Serikali na kuwa imefika wakati ofisi za Serikali zimehamia hotelini, lengo likiwa ni watumishi wa umma kutafuta mwanya wa kulipana posho.

“Ndiyo maana watu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wanakusanya fedha nyingi, lakini ni fedha kidogo sana zinazokwenda kwenye huduma za jamii. Nadhani hili ni tatizo na ni utawala mbaya kabisa, lazima kuwepo mabadiliko kama kweli tunataka kuisaidia nchi yetu,” alisema Sumaye.

Kuhusu posho za wabunge, Sumaye alisema ni jambo la hatari kwani ikiwa wabunge watalipwa viwango vya posho vilivyotangazwa, linaweza kuvuruga amani ya nchi.

***Ndungai ajibu mapigo

Akijibu kauli iliyotolewa na Bw. Sumaye Naibu Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai alilifananisha posho hiyo na tone la maji ikilinganishwa na mamilioni ambayo alidai vigogo wa mihimili mingine ya dola wanalipana.

Alisisitiza kuwa posho hizo hazilingani kwa namna yeyote ile na posho wanazopewa viongozi wastaafu serikalini na wale wa Mahakama.

Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa posho wanazolipwa wabunge ni kidogo ikilinganishwa na mihimili mingine ya dola.

Alisema pia mishahara ya wabunge ni tone tu la mshahara wa ofisa wa kawaida wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisa wa ngazi ya chini wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

“Wenzetu wa Kenya na Mauritius wana tume ambayo ni huru na ina watu ambao wanaaminika kuwa ni waadilifu, ndiyo wanaangalia mishahara ya viongozi wa juu kama hapa kwetu labda ni kuanzia kwa mkuu wa mkoa mpaka hata Rais. Ukienda kwenye mtandao unaona kila kitu, hakuna usiri, tupate chombo huru ambacho kitatupangia sisi wote ambao tunapata pesa kutokana na kodi za wananchi... nasema Watanzania wangejua maeneo mengine kukoje wangeachana kabisa na suala la posho za wabunge.”

Kwa sasa inakadiriwa kuwa kila mbunge analipwa zaidi ya sh. milioni 7 kila mwezi, ikiwa ni mshahara pamoja na posho nyingine.

4 comments:

  1. Kuwa na tume ya kupanga mishahara ya watumishi wa umm ni jambo zuri. Lakini kwa nini watu kama Mwakapugi ambao majina yao yaliwahi kutajwa kwenye tuhuma fulani wawekwe humo kama vile watanzania ni wameisha?

    ReplyDelete
  2. Tume isije kuwa danganya toto huku ikitimiza matakwa ya wakubwa tu!

    ReplyDelete
  3. Tulikuwa na Tume iliyoangalia maslahi ya watumishi iliyoongozwa na Mh Deogratius Ntukamazina sasa Mbunge wa Ngara katika awamu hii ya nne kuangalia malipo ya mishahara ya watumishi wa umma. Je yale mapendekezo yameishia wapi.
    Tusitumie tume kama mbinu ya ucheleweshaji wa kutatua matatizo katika maslahi ya watumishi wa umma na wastaafu. Malipo ya watumishi wa umma yaendane na hali ya maisha kwa kipindi husika.
    Malipo ya mishahara na pensheni za watumishi ziendane na thamani ya dola ya Marekani kwa kipindi husika. Kwa mfano kama mshahara wa mtumishi kwa mwezi au malipo ya pensheni kwa watumishi waliostaafu yawe yanalingana na dola kwa mshahara wa mtumishi kwa mwaka husika na mstaafu anapostaafu. Kwa mfano mtumishi aliyelipwa pensheni ya kila mwezi ya shs 2000 wakati thamani ya dola ilikuwa tshs 8/= aendelee kulipwa kiasi hicho hicho hata shs ya Tanzania inaposhuka thamani.
    Kwa mstaafu aliyetajwa hapo juu anatakiwa alipwe dola 250 kwa mwezi kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ilivyo kwa sasa. Hii itafanya malipo ya pensheni kwenda sambamba na thamani ya dola kwa shilingi ya Tanzania kwa wakatihusika. Itakuwa inalingana na kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola ya Marekani.

    ReplyDelete
  4. IKIWA SERIKALI INALIBANA BUNGE KUHUSU POSHO NA BUNGE NALO LIAMKE LIANZE KUIBANA SERIKALI AMBAYO IMEJAA WIZI, RUSHWA, UFISADI, UVIVU, KUTOKUWAJIBIKA, MIGOMO UPOTEVU WA FEDHA NYINGI.

    BUNGE LINAO UWEZO MKUBWA SANA KIKATIBA WA KUITHIBITI SERIKALI KWA KUWA WAO WANAWAWAKILISHA WENYE SERIKALI AMBAO NI WANANCHI. WASIOGOPESHWE AU KUKEMEWA NA SERIKALI WAKAE BUNGENI WACHAMBUE MASUALA KWA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI.

    SERIKALI HAIWEZI KUCHOCHEA UA KUWASHAWISHI WNAINCHI WAWACHUKIE WABUNGE WALIOWACHAGUA KWA KUJARIBU KUFICHA MADAHAMBI YAO.

    WABUNGE WAKIFUATILIA WIZI SERIKALINI KAMA WA EPA, RICHMOND, MIKATABA MIBOVU YA MADINI N.K. wAKIPIGA MAHESABU, WATAPATA FEDHA NYINGI ZA KUWALIPA HATA ZAIDI YA KIMA CHA POSHO WANACHODAI KWA SASA. TIJA SERIKALINI ITAONGEZEKA NA UCHUMI UTAKUA KWA KASI ZAIDI. WANANCHI, WATUMISHI SERIKALINI WATANUFAIKA HIVYO KUWAPENDA WABUNGE.

    ReplyDelete