*Mechi yao yaingiza mil. 268/-
eki wa timu ya ES Setif ya Algeria, Smain Diss (katikati) akimdhibiti mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu (kushoto) huku Haruna Moshi 'Boban' akiambaa na mpira wakati timu hizo zilipoumana katika mechi ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi.Simba ilishinda mabao 2-0.(Picha na Imma Mbuguni).
Na Elizabeth Mayemba
BAADA ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya ES Setif ya Algeria, Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amesema mwanzo umekuwa mzuri kwao, lakini wana kazi kubwa katika mchezo wa marudiano kutokana na ubora wa wapinzani wao.
Katika mchezo huo wa juzi, mshambuliaji wa timu hiyo Emmanuel Okwi na kiungo Haruna Moshi 'Boban' ndio waliokuwa mashujaa katika mchezo huo na kuiweka timu yao nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho (CAF).
Akizungumza juzi mara baada ya mchezo huo kumalizika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Milovan alisema amefurahi kupata ushindi huo na kutoruhusu kufungwa, lakini pia amekiri kwamba bado wana kibarua kigumu mechi yao ya marudiano itakayochezwa wiki mbili baadaye, kutokana na kiwango cha juu kilichooneshwa na wapinzani wao.
"Kwanza nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi mzuri walioupata, bado kuna upungufu, hivyo nitaufanyia kazi kwani katika mechi ya marudiano tutakuwa na kazi kubwa, timu ES Setif si timu ya kuibeza," alisema Milovan.
Alisema mechi hiyo imetoa mwanga kwa wachezaji wake kwani wameshatambua aina gani ya timu wanacheza nayo kutoaka na awali kutoijua vizuri, hivyo ni wakati wao wa kuangalia ni wapi wanatakiwa kujirekebisha.
Milovan alisema washambuliaji wake, Okwi na Felix Sunzu hawakuonekana sana kwa kuwa wapinzani wao walikuwa wanajua ubora wao na ndio maana waliwakaba sana.
Katika hatua nyingine, mechi ya Simba dhidi timu hiyo, imeingiza sh. 268, 539,000 kutokana na idadi ya tiketi kwa gharama tofauti tofauti 43, 592,000.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilieleza kwamba mapato hayo yanaonekana ni tofauti na idadi ya watu walioonekana wameingia uwanjani.
Katika mechi hiyo viingilio vilikuwa ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B na sh. 25,000 kwa VIP A.
Hongera MNYAMA. kaza buti safari ndo kwanza imeanza
ReplyDelete