23 March 2012

Chadema kuanza kampeni kwa helikopta Arumeru

*Ni kwa helkopta, Dkt.Slaa asema akitaeleweka
Na Queen Lema, Arumeru

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Willibrod Slaa amesema kuwa watalazimika kufanya kampeni kutumia usafiri wa anga wa helikopta katika Jimbo la Arumeru Mashariki kwa vile lina vijiji vingi huku muda wa kampeni unakaribia kumalizika.

Dkt. Slaa aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Ngurdoto. Alisisitiza kuwa katika uchaguzi huo Chadema itafikia viji vyote.

Alisema muda wa kampeni ulipangwa mdogo ili Chadema usifike katika baadhi ya vijiji. Aliwahakikishia wananchi kuwa hakuna
kijiji ambacho chama hicho kitashindwa kukifika.

“Sasa hivi tutafika kila mahali kwa kutumia helikopta (Chopa)na kitu
ambacho mimi najua ni kuwa CCM inaona kuwa tunaweza tusifike katika
sehemu zote ndio maana hata muda wa kampeni ukawa ni mfupi, lakini
hatujali kabisa hilo,” alisema Dkt. Slaa.

Katika hatua nyingine mgombea wa chama hicho Bw. Joshua Nassari, alimtaka Mbunge wa Korogwe, Bw. Stephen Ngonyani (Profesa Maji Marefu) aache kueneza propaganda mbaya dhidi yake na badala yake anatakiwa kujua na kutambua kuwa anaongozwa na Mungu.

Bw Nassari alisema kuwa ndani ya wiki hii mbunge huyo amejitangazia
kuwa ametiwa maisha jambo ambalo si la kweli.

Aliongeza kuwa mbunge huyo ndiye alikwenda kwenye ngome ya chama chake bila kueleza shida yake.

“Huyu Majimarefu ametengenezewa picha za kwenye magazeti
wakati amekuja katika ngome yetu bila ya sisi kujua amefuata nini,
halafu pia anasema kuwa nimemtishia ni wapi tulikutana? Anatakiwa kujua kuwa sisi tunasonga mbele hatuangalii propaganda kama hizo na badala,” aliongeza Bw. Nassari

Katika hatua nyingine Chadema kimesema njia ya kisayansi ambayo kinaitumia katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, imefanikiwa kugundua mbinu mbalimbali za wizi wa kura ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo feki katika baadhi ya vijiji.

Dkt. Slaa alisema kupitia mbinu hiyo ya kisayansi ambayo wanaitumia ili kuepukana na wizi wa kura halali za wagombea wa chama
hicho, wamefanikiwa kujua idadi kubwa ya vituo feki, ambavyo vimewekwa kama njia ya kuongeza idadi ya kura.

Alibainisha kwamba kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, msimamizi wa uchaguzi anapaswa kushirikisha wadau hasa pale ambapo kuna kuwa na umuhimu wa kuongeza vituo, lakini hajafanya hivyo na badala yake vituo hivyo vimeongezwa kwa siri.

“Mbinu ambayo Chadema tunaitumia ni kali sana na tumeweza kujipenyeza
hadi CCM na tumefanikiwa kupata hii karatasi ambayo inaonesha wazi
kuwa wameipata wiki, sasa na sisi hatujapewa kabisa kutokana na
hali hii inaonesha jinsi Tume (Tume ya Taifa ya Uchaguzi)ilivyojipanga na hivi vituo feki na wameviongeza kwa misingi gani hapa, tutapambana,” alisisitiza Dkt. Slaa.

Kutokana na hali hiyo Dkt. Slaa alisema kuwa ndani ya uchaguzi
mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki ni lazima amani na haki viwepo,
lakini kama haki itakuwa inaibiwa kwa misingi ya ujanja ujanja ni wazi
kuwa Arumeru itabadilika kuwa kama Tunisia kwa kuwa chama hicho kwa
sasa hakipo tayari kuonewa na kuibiwa kura.

Awali alisema kuwa anataka majina ya wapiga kura yabandikwe haraka
iwezekanavyo kwa kuwa ni haki kwa mujibu wa sheria.

Alisema kutokana na hali hiyo kila mpiga kura atabaini hata kama hakuna jina lake jambo ambalo litafanya mpiga kura kupata msaada haraka sana.

Aliongeza kuwa endapo tume kupitia kwa watendaji wake,
haitaweka majina ya wapiga kura siku ya leo ni wazi kuwa
atapambana kwa ukali.

Alifafanuwa kuwa mara nyingi wapiga kura hawapigi kura kutokana na kutokuwepo kwa majina yao.

Kwa upande wake mgombea ubunge kupitia chama hicho Bw. Nassari, alisema kamwe mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM asijifananishe naye kwa kuwa yeye anajua kero za wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Bw Nassari alifafanua kuwa yeye ni sawa na "Dogo Janja" wa mjini na kwa hali hiyo yupo tayari kufanya kazi katika maeneo yoyote yale.

No comments:

Post a Comment