Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga wamedai kusikitishwa na kitendo cha Serikali kumsamehe katika mazingira ya kutatanisha wakala aliyekamatwa na wananchi akiwa na mbegu za pamba zilizooza.
Madiwani waliyasema hayo mwishoni mwa wiki baada ya kupokea taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bw.Ally Rufunga ambapo alisema, Kampuni ya Alliance iliyokuwa ikituhumiwa kwa kosa la kutaka kusambaza mbegu mbovu kwa wakulima ilisamehewa kwa agizo kutoka ngazi za juu.
Bw.Rufunga alitoa taarifa hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika hivi karibuni mjini Mwanhuzi ambapo alisema, msamaha huo uliotolewa kwa kampuni hiyo kwa kuzingatia mchango wake katika suala zima la ununuzi wa zao la pamba.
“Ni kweli wakala huyu alisamehewa, hii ni kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ana kumbukumbu nzuri katika utendaji wake sambamba na kuwa kampuni pekee iliyonunua pamba kwa bei ya juu kiasi cha shilingi 1,400 wakati kampuni nyingine zilinunua kwa bei ya shilingi 800 kwa kilo moja.
“Kutokana na hali hiyo uongozi wa Bodi ya Pamba uliagiza zitumike busara katika kosa alilokuwa ametaka kulifanya, ambapo pamoja na msamaha huo, lakini alipewa adhabu ya onyo la maandishi, hivyo iwapo atarejea tena ndipo atakapochukuliwa adhabu nyingine,” alisema Bw. Rufunga.
Hata hivyo wakati madiwani wakichangia hoja hiyo mbele ya mkuu huyo wa mkoa walionesha wazi kutoridhishwa na msamaha huo ambapo walidai kuwa kitendo cha kumsamehe wakala huyo kwa kigezo cha kuwa na kumbukumbu nzuri za nyuma kitawavunja moyo watendaji wa ngazi ya chini walioshirikiana na wananchi kumkamata.
Diwani wa Kata ya Mwabuzo, Bw.Seni Chalya alisema, anapata wasiwasi kwa jinsi hali ya mambo inavyokwenda kutokana na hoja za pamba kwa kipindi kirefu kutopatiwa ufumbuzi na kila linapojitokeza tatizo watu huelezwa kwamba kuna maelezo yametoka ngazi za juu hivyo mambo yanamalizwa kienyeji.
“Tumeamua kuilinda Katiba yetu, tuliapa, sasa hawa wamefanya makosa, inakuwaje wanasamehewa kienyeji, huo ni uvunjaji wa Katiba, je mwananchi wa kawaida akifanya hivyo itakuwaje? Wananchi na watendaji waliomkamata watatuelewaje?.
“Tukiendelea na tabia hii hatutafika mahali popote, watendaji wa vijiji waliofanya kazi hiyo wakiisikia taarifa hii watajisikiaje? Wanakamata magari, lakini ghafla inatoka ‘order’ kutoka juu kwamba huyo mwachieni, hali hii inatupa wasiwasi,” alisema Bw.Chalya.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw.Pius Machungwa alikanusha madai ya Kampuni ya Alliance kununua pamba kwa bei ya sh. 1,400 ambapo alisema, kampuni iliyonunua bei ya juu ilikuwa ni Biore ambayo ilinunua kwa sh. 1,280 na hakuna kampuni nyingine iliyofikia kiwango hicho.
Hata hivyo kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi, Bw.Simon Hyagila alisema, tatizo la usambazwaji wa mbegu za pamba zilizooza limesababishwa na wakulima wenyewe kutokana na kuuza pamba iliyochanganywa maji na magadi.
HII HALI NDIYO TULIYO ITAKA SISI WASUKUMA NA UJINGA WETU WA KUCHAGUA CCM KILA MARA.NDUHU SHIDA HUKU TUNAUMIA. NANI KATOA HUO MSAMAHA? TUNAONEKANA SISI NI WATU WA KUPANDIWA NGAZI HATA NA WAPUMBAVU. HUO NI WIZI WA HALI YA JUU. MNATISHIWA SERIKALI,NANA SERIKALI ZAIDI YA WANANCHI? MADIWNI MSIKUBALI.TUANDAMANE JAPO WENGINE WAJINGA WATASEMA MIMI CHADEMA. SI KWELI.UONEVU HUU MPAKA LINI?MBONA MIKOA ILIYONA WASOMI WENGI HAKUNA HUU UPUUZI KAMA HUKO KWETU USUKUMANI?
ReplyDelete