13 February 2012
Mtumbwi wasababisha maafa kisiwani Pemba
Na Juma Mussa, Micheweni
WATU wawili wamefariki dunia na wegine kadhaa kunusurika katika ajali ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria baada ya kupiduka katika Bahari ya Hindi.
Ajali hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Kipange Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba majira ya usiku.
Hata hivyo waliofariki dunia ni mwanafunzi, Bani Khamis Juma (18) darasa la sita, Said Hamad Abdalla (12) darasa la tatu wote kutoka Shule ya Msingi Kipange Konde ambapo walikuwa wakisafiri kutoka kijijini kwao kuelekea Kijiji jirani cha Gando.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Bugi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba chanzo chake kilitokana na mtumbwi huo kukumbwa na upepo hivyo kupinduka katika kivuko baina ya vijiji hivyo viwili.
"Tayari polisi wametumwa ili kuangalia kama kuna watu wengine waliozama, watu hao walikuwa wakielekea Kijiji cha Gando kwa sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume SAW, na maiti zote mbili zimeshapatikana hivyo tayari zimeshafanyiwa taratibu za mazishi.
"Hakuna taarifa kamili ya idadi ya watu waliokuwemo kwenye mtumbwi huo na tunaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo,"alifafanua Kamanda huyo.
Katika siku za hivi karibuni mwambao wa Bahari ya Hindi umekuwa ukikumbwa na upepo wenye mawimbi makali ambao mara kwa mara umekua ukisababisha maafa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment