Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
IMEELEZWA kuwa upimaji wa ardhi katika Mkoa wa Kilimanjaro ni njia pekee
ambayo inaweza kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi ambalo limekuwa kikwazo mkoani humo kwa muda mrefu hali ambayo inasababishwa na uhaba wa ardhi.
Hata hivyo wananchi mkoani humo wamekuwa wakiingia kwenye matatizo ya migogoro ya ardhi ya mara kwa mara kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu wa kupima viwanja sambamba na umiliki wa hati.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Upimaji
Ardhi na Uendelezaji wa Makazi (Nice Estate Agency), Bw.Evans Ngolly wakati wa uzinduzi wa kampuni hiyo mkoani Kilimanjaro.
Alisema, ni vema wananchi wakajiwekea utaratibu wa kupima maeneo yao ili
kuepuka matatizo ya migogoro ya mara kwa mara isiyo na lazima katika jamii
hali ambayo imekuwa ikichangia kurudisha nyuma jitihada za kujiletea
maendeleo.
“Kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Kilimanjaro
ndiyo maana tumeamua kufungua tawi, katika mkoa huu ili kuleta huduma karibu
kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa manispaa zetu hazina uwezo wa kifedha
na nguvu kazi,”alisema Bw.Ngolly.
Bw.Ngolly alisema, upimaji huo wa ardhi utasaidia kuharakisha mchakato wa Mji wa Moshi kuwa jiji kutokana na kwamba kumekuwepo na mvutano uliosababishwa na wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha na wengi
wakijikuta wakigoma kuachia maeneo yao.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa urasimishaji wa maeneo ya ardhi yanayomilikiwa pamoja na migogoro ya ardhi wanayokutana nayo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bw. Mussa Samizi alipongeza hatua za kampuni hiyo na kwamba Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati katika kufanikisha shughuli za upimaji viwanja na utoaji hati miliki.
Bw.Samizi aliwataka wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kupima ardhi
zao ili kuweza kupata hati miliki na kuondokana na matatizo ya migogoro ambayo yamekuwa yakichangia kuzorotesha shughuli zao za maendeleo.
“Naomba niipongeze sana kampuni hii, kwani imekuja wakati muafaka, wakati
ambao manispaa yetu ya Moshi ipo kwenye mchakato wa kuwa jiji tunaamini
kabisa kuwa mtatusaidia kupima ardhi na kuwezesha kuwa kwenye utaratibu
unaoeleweka,”alisema Bw.Samizi.
No comments:
Post a Comment