13 January 2012

Wakuu wa miradi wapigwa msasa

Na Pamela Mollel,
Arusha

SERIKALI imeazimia kuboresha mfumo wa usimamizi wa fedha za umma na kutekeleza mipango iliyojiwekea kikamilifu ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho makubwa kupitia mfumo wa fedha(IMFS) ili kupunguza changamoto zilizojitokeza kwa miaka kumi ya utekelezaji wa mfumo wa 'Epicor 9.05' kwenye
baadhi  halmashauri  zake.


Akifungua mafunzo hayo jana Jijini Arusha kwa wakuu wa idara na wasimamizi wa miradi wa halmashauri Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bi. Eveline Itanisa alisema kuwa
mafunzo hayo yataweza kuboresha hali ya utendaji katika halmashauri hasa kwenye upande wa usimamizi wa fedha za umma.

Bi.Itanisa alisema kuwa mfumo huo ulioboreshwa wa Epicor 9.05 unaunganisha halmashauri zote nchini katika kompyuta kuu ambapo utazingatia na kwenda
sambamba na maamuzi ya serikali ya kupunguza idadi ya akaunti za Halmashauri na kufikia akaunti sita (6) tu.

Alisema mfumo huo mpya utaweza kuthibiti matumizi mabaya ya fedha na kufuatilia kinachoendelea kwenye mfumo  ikiwa ni pamoja na kupata taarifa muhimu kuhusu maeneo yao toka kwenye mfumo huo muda wowote.

Naye mwezeshaji wa kitaifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Bw.Jeremia Ezekiel Mtawa amebainisha kuwa lengo hasa la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wakuu wa idara na
wasimamizi wa miradi kusimamia fedha zao katika mfumo huo mpya.

Bw.Mtawa aliongeza kuwa mfumo uliokuwa ukitumika awali ulikuwa hautoi taarifa kwa wakati na wakati mwingine taarifa hizo zilikuwa sahihi lakini hazifanani.

No comments:

Post a Comment