13 January 2012

Kijiji kutumia mil 60/- kujenga zahanati

Na Thomas Kiani
Singida

UJENZI wa Zahanati ya kisasa katika Kijiji cha Nsonga Kata ya Kaselya wilayani Iramba mkoani Singida unahitaji sh. milioni 60 pamoja na nguvu kazi ya wakazi wa eneo hilo na serikali.


Akizungumza na Majira juzi ofisini kwake Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Bw. Mohamed Mkanga alisema kijiji chake kilifikia uamuzi wa kujenga zahanati nzuri ya kisasa yenye hadhi yake mwaka 2007 kwa kutumia michango na nguvu za wananchi hadi
ujenzi wake utakapokamilika.


Bw.Mkanga alisema zahanati hiyo inategemewa kutoa huduma zake kwa wananchi wa kijiji hicho na vile vya jirani na hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo ya kiafya kwa wananchi wote.

Aliongeza kusema kuwa jengo la kliniki limejengwa tayari bado nyumba ya Mganga na vyoo viwili ya zahanati hata hiyo amedai uchangiaji wake kutoka kwa
wananchi umekuwa mdogo kwa sababu hawana mwamko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Idd Mkumbo alisema serikali imechangia fedha za ujenzi wake na imeahidi kuendelea kuchangia na kutoa samani hadi itakapofunguliwa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Bw. Lameck Mwigulu alichangia fedha za ujenzi wake na ameahidi kuendelea kuchangia kwa malengo ya wananchi  wa kijiji hicho wapate huduma za afya zinazotakiwa za kimsingi kwa ukaribu zaidi hasa watoto wadogo na akina mama wajawazito.

Kijiji cha Nsonga chenye watu 2347 idadi iliyotolewa na sensa mwaka 2002 wakiwa wakulima na wafugaji waliamua kutenga eka 5 kujenga zahanati, kliniki na nyumba ya Mganga hii ni kwa sababu ya kuondoa matatizo ya kupata huduma za kiafya.


 

No comments:

Post a Comment