05 December 2011

Gari la Ofisa Ulinzi rasilimali za nchi lachomwa moto

Na Livinus Feruzi, Bukoba

SIKU chache baada ya kikosi cha ulinzi wa raslimali za uvuvi Kanda ya Kagera kufanikisha kukamatwa kwa tani tatu za samaki wachanga zikiwa katika harakati za kusafirishwa kwenda nje ya nchi, watu wasiofahamika wamevunja nyumba ya Ofisa mfawidhi wa kikosi hicho Bw.Rodrick Mahimbali, kisha kuchoma moto gari lake.

Tukio hilo linalohusishwa na juhudi za Ofisa huyo kusimamia rasilimali za nchi lilitokea usiku mwishoni mwa wiki iliyopita saa tisa usiku akiwa amelala baada ya watu wasiojulika kuchimba na kufanikiwa kuvunja kisha kuingia kwenye banda la gari na kulichoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli.

Akizungumzia tukio hilo Bw. Mahimbali alisema kabla ya watu hao kulichoma moto
gari hilo ambalo lilikuwa karibu na chumba alipolala walianza kulimwagia mafuta ya petroli hivyo kumshutua na kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani.

Alisema kelele hizo zilimsaidia kwa kuwaamsha majirani waliofika na kufanikisha kuzima moto kabla ya kuleta madhara makubwa ikiwemo kuteketeza
gari hilo na kuunguza nyumba nzima.

Ofisa huyo alisema kinashomshtua ni kuwa tukio la gari lake aina ya Toyota kuchomwa moto limekuja siku chache baada ya serikali kuongeza nguvu katika ulinzi na udhibiti wa raslimali za uvuvi kutokana na kubainika kwamba samaki
wachanga wanapelekwa nchi jirani hivyo kuikoseha taifa mapato.

“Kwa siku 10 tangu tarehe 20 mwezi Novemba hadi 30 tumefanikiwa kukamata
takribani tani tatu za samaki wachanga na mabati mawili yaliyokuwa na
makontena ya kukusanyia samaki kinyume cha sheria, hii inatokana na
ukweli kwamba wavuvi wa Tanzania wanashirikiana na waganda kuhujumu nchi,” alisema na kuongeza.

“Udhibiti wa uvuvi haramu kwa nchi jirani ni hafifu, samaki kwao wameisha waganda wapo tayari kununua samaki kwa bei kubwa mara mbili ya Tanzania maana wanachotaka ni samaki,”alisisitiza.

Hata hivyo alisisitiza kuwa licha ya tukio hilo baya kwake la gari lake kuchomwa moto haliwezi kumzuia kutekeleza majukumu yake na kuwa hizo ni changamoto za uwajibikaji katika kutimiza wajibu hivyo ataongeza bidii zaidi katika operesheni hiyo.

Aliwataka maafisa uvuvi wa halmshauri za wilaya zote za Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanashiriki kulinda raslimali za uvuvi ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria na kanuni za uvuvi kwa kuwa sekta ya uvuvi ni chanzo kikubwa cha mapato ya halmashauri husika na serikali kwa ujumla kama utasimamiwa vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Bw. Henry Salewi, alithibitisha kuwepo kwa
tukio hilo na kuongeza kuwa polisi wanaendelea na juhudi za kuwatafuta
wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

2 comments:

  1. Msiache kuwa makini kukamata wanaohujumu uchumi wa nchi hata kidogo

    ReplyDelete
  2. watu hawa wanaohujumu mapato ya taifa wasiachwe bila kupewa faini maradufu ya vile ambavyo wanafikiri wangepata faida kubwa ili wapate kujaza matumbo yao.

    ReplyDelete