Na Peter Mwenda, Kibaha
MPANGO wa Taifa wa Damu Salama Tanzania umetoa wito kwa watanzania kujitolea kutoa damu kwa hiari kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kwa dharura
katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ambako wadau wakubwa wa wanaojitolea ambao ni wanafunzi wanakwenda likizo.
Meneja wa Mpango Taifa wa Damu Salama Tanzania, Dkt. Afespa Nkya, alitoa wito huo wakati akihitimisha warsha ya Kikosi kazi cha mpango huo na kuviomba taasisi za dini, vikundi vya kijamii na asasi mbalimbali kujitokeza kuokoa maisha ya watanzania wenzao kwa kujitolea damu.
"Hali ya uchangiaji damu katika kipindi hiki ambacho shule na vyuo vimefungwa na watu wanajiandaa kwa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ni mbaya, ni vizuri sehemu za ibada, sokoni na kwenye mikusanyiko ya watu wajitokeze kutoa damu kuokoa maisha ya watanzania wanaohitaji huduma hiyo kwa dharura," alisema Dkt. Nkya.
Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watu zaidi ya watu milioni 40 na kwamba ikiwa watu 450,000 wakijitokeza kutoa damu hakutakuwa na upungufu kwa mwaka mzima kwa kuwa mahitaji ya damu ni uniti 350, 000 hadi uniti 400,000 kwa mwaka.
Dkt. Nkya alisema hakuna njia mbadala ya kupata damu zaidi ya watu kujitolea kusaidia wengine wanaohitaji na kwamba kila Mtanzania ambaye yuko tayari kutoa damu anatakiwa kwenda katika vituo kimojawapo kati ya saba ambavyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Tabora, Hospitali ya Jeshi Lugalo pamoja na Mtwara.
Pia alitaja vituo vidogo vya kujitolea damu chini ya mpango huo kuwa ni Mnazi mmoja Dar es Salaam pamoja na Dodoma.
Alisema wizara ya Afya na Ustawi wa jamii imetoa waraka kwa hospitali zote nchini kuwa mwananchi anapotakiwa kununua damu atoe taarifa Makao Makuu ya wizara na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa huduma hiyo hutolewa bure bila malipo yoyote.
Alisema mpango huo umeweka mikakati ya kukabiliana na majanga kama lililowahi kutokea mwezi Februari mwaka huu ya mlipuko wa mabomu kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto.
Awali Mwenyekiti wa kikosi kazi, Bw. John Bwire, alisema Mpango wa Taifa wa Damu salama ushirikiane na waandishi katika kampeni ya kutoa elimu kwa watanzania kuhusu huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment