14 November 2011

MAONI YA KAFULILA KUHUSU MAMLAKA YA RAIS MCHAKATO WA KATIBA MPYA.

Jana wakati nachangia kwenye mjadala wa wabunge wote kuhusu namna ya kuenenda katika mjadala wa katiba nilijaribu kuweka msimamo wangu wa ujumla kuhusu misingi ya kufanya mjadala huu ufike salama na kufikia matokeo tunayotaka kama Taifa.
Msingi huo ni Trust(imani). Hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa sasa imepunguza kiasi kikubwa cha kuaminiana. Na hii sio Tanzania tu bali nchi nyingi masikini duniani. Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ndugu Ban Ki Mon akifungua mkutano wa Bunge la Dunia Oktoba 15, 2011 alisema TATIZO KUBWA KWA NCHI MASIKINI DUNIANI SASA SIO NAKISI YA BAJETI(BUDGET DEFICT) BALI NAKISI YA IMANI YA UMMA KWA WATAWALA(TRUST DEFICIT) NA UFUMBUZI WA TATIZO HILI NI UWAZI NA WATAWALA KUKUBALI MAMLAKA YA UMMA...

Tatizo la umma kupoteza imani kwa watawala ndio msingi hata wa kuhitaji katiba mpya, mana zamani enzi za Mwalimu Nyerere Katiba ilikuwa mbaya kuliko tuliyonayo leo,ilifika mahala Mwalimu Nyerere akasema hii katiba inamtosha Rais kuwa Dikteta lakini kwakuwa Umma uliamini kwa waliopewa madaraka hoja ya katiba haikuwa agenda..

Huu ndio msingi wa msimamo wangu kusisitiza umuhimu wa kupunguza mamlaka ya Rais katika mchakato huu. Baadhi ya maeneo ambayo nashauri yatazamwe ili kupunguza mamlaka ya Rais ni pamoja na;

KUHUSU TUME

1.Ibara ya 5 ya muswada inaeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar ndiye mwenye mamlaka ya Kuunda Tume. Mimi nashauri Rais apendekeze majina ya wajumbe wa Tume yatangazwe gazeti la Serikali uwepo muda wa Umma kutafakari majina hayo na kisha yapitishwe na Bunge.

Pia kwenye kuwaondoa isiwe kama inavyotamkwa ibara.........kwamba wakifanya makosa wanaondolewa bila mchakato mgumu wa kumwondoa. tuweke mchakato mgumu kama ilivyo kwa majaji, kwamba kumwondoa mjumbe Rais atoe pendekezo na kiwepo chombo cha kupitia pendekezo hilo ili kuthibitisha uamuzi wa Rais kumwondoa mjumbe husika.

Tukifanya hivi tutakuwa tumeihakikishia Tume mamlaka na Uhuru wa kutosha kuweza kufanya kazi bila hofu ya aliyewateua.Lakini kubwa zaidi utaratibu huu utaijengea Tume uhalali wa kisiasa(political legitimacy) kwamba Umma una imani na Tume. Hiki ni kitu muhimu sana.

2.Ibara ya 8(1) Hadidu za rejea kutolewa na Rais kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar. Hapa panaweza kuwa na hofu ya Rais kuamua matokeo ya maoni kutokana na mfumo wa hadidu atakazotoa. Hadidu za rejea ni kitu kikubwa sana kwenye kuamua matokeo ya kura ya maoni.

Hivyo ni muhimu Hadidu za rejea ziwe sehemu ya sheria kabisa kuondoa hofu hiyo. Hadidu za rejea zikiwa sehemu ya sheria sio rahisi kuchezewa na mamlaka yoyote bila utaratibu wa sheria kufuatwa.

SEKRETARIET YA TUME

Ibara ya 13(2) Rais atateua Katibu wa Sekretariet ya Tume.Hiki ni chombo cha kiutendaji chini ya mamlaka ya Tume. Kama Tume itapatikana kwa namna niliyoeleza hapo juu, nashauri sekretariet ya Tume iteuliwe na Tume yenyewe kwa kuzingatia vigezo ilikuifanya sekretariet iwajibike kwa Tume na kuepusha nguvu na mamlaka za Rais katika shughuli za utendaji wa Tume.Hapa nazingatia uzoefu wa Sekretariet ya Tume ya Pro Shivji ambapo analalamikia uzembe kutokana na Tume kukosa mamlaka ya kuidhibiti.

Ibara ya 13(5) Inaelezwa kuwa wajumbe wa Tume na Sekretariet watalipwa na Waziri ambaye ni mteule wa Rais kadiri atakavyo amua kulingana na sheria na kanuni za nchi. Hapa nashauri viwango na utaratibu wa malipo viwekwe wazi, na kuondoa uwezekano wa serikali kuamua mwelekeo wa kiutendaji wa Tume kwakuwa majaaliwa ya utendaje yamefungwa mikononi mwa wizara. ni muhimu uwepo mfuko maalumu kwa kazi hii kuepusha visingizio vya sababu za kibajeti kuathiri utendaji wa Tume. Hapa tunao uzoefu mzuri wa nchi ya Uganda ambapo Serikali iliyumbisha mchakato wa katiba kwasababu za kibajeti kwa malengo ya kisiasa.
 
Ibara 18(1). Inasema baada ya Tume kukamilisha kazi yake itawasilisha ripoti kwa Rais na Rais wa Zanzibar na Ibara ya 18(2) inasema Baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar na baada ya kukamilisha majadiliano kuhusu masuala ya kisera, taratibu  na kiutendaji, Rais atamwagiza waziri kuwasilisha muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba na Ibara ya 26(2) kinasema Baada ya kuvunjwa Bunge la Katiba bado Rais anayo mamlaka ya kuliitisha Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale siku zijazo kwa ajili ya kutunga masharti ya katiba kabla ya kuzindua katiba inayopendekezwa kwa lengo la kuboresha masharti yaliyomo kwenye katiba inayopendekezwa.  Haya ni maeneo yanayo onesha mamlaka ya Rais kuamua katiba iwe ya namna gani. Kwanza Bunge likipitisha katiba inayopendekezwa haifai Rais tena aboreshe na badala yake katiba inayopendekezwa inapaswa kupelekwa kwa wananchi. Pili, Baada ya Tume kukamilisha kazi yake haipaswi kuwasilisha ripoti kwanza kwa Rais, inapaswa kwanza iwasilishwe kwa wananchi kwa kuchapwa kwenye gazeti na uwepo muda umma kujiridhisha kama hicho kilichochapwa ndio maoni yao?.. na ndipo ripoti akabidhiwe Rais.. Mwenyekiti wa Tume ndiye anaepaswa kuwasilisha ripoti ya Tume kwenye Bunge la Katiba badala ya Waziri..Hii ni kwasababu ripoti sio ya serikali ni ya tume lakini pia Mwenyekiti wa Tume ndiye aliyeshiriki mchakato wa kukusanya maoni hivyo anao uwezo na mamlaka ya kujibu hoja za wabunge wa Bunge la Katiba kuhusu ripoti yake.
 
Ibara ya 20(1) Inasema Rais ataunda Bunge la Katiba, Pia 20(4) Rais ndiye atakayeteua wajumbe 116 kutoka Taasisi za kidini, asasi zisizo za kiserikali, vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalumu katika jamii.  Hapa kwanza nashauri tuondoa kabisa dhana ya Rais kuunda Bunge la Katiba kwa ujumla wake. Pia kama haiwezekani kuendesha mchakato wa uchaguzi kupata wabunge wa Bunge la katiba kwa nchi nzima, bado wajumbe waliobanishwa kutoka taasisi tajwa hapo juu wasiteuliwe na Rais moja kwa moja, badala yake taasisi tajwa zipewe mamlaka ya kuchagua wajumbe wa kuwakilisha taasisi husika kwenye Bunge la Katiba. Hii itazipa mamlaka taasisi hizo kuamua mtu sahihi ndani yao badala ya kuamuliwa na Rais. 
 
Mwisho mchakato wa kura ya maoni kwa mujibu wa muswada  utaendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Lakini Umma hauna imani na Tume ya Uchaguzi kutokana na namna inavyo undwa na kufanya kazi. Tume tuliyo nayo bado inaonesha mamlaka ya Rais kuamua, hivyo ni muhimu kupata Tume mpya itakayopata uhalali wa kisiasa kuweza kusimamia kura hiyo ya maoni kuondoa uwezekano mkubwa wa wananchi kupinga baadhi ya matokeo kwa kigezo cha imani ya umma kwa Tume.
 
HAYA NI BAADHI YA MAENEO YANAYOPASWA KUREKEBISHWA KUPUNGUZA MAMLAKA ZA RAIS NA KUONDOA MCHAKATO WA KATIBA MIKONONI MWA DOLA KUWAit MIKONONI MWA UMMA.

No comments:

Post a Comment