14 November 2011

Kamati ya Majadiliano imechangia kuharakisha maendeleo - Kombani

 na Godfrey Ismaely, Dodoma

SERIKALI imesema jitihada za kuishirikisha Kamati ya Majadiliano kabla ya kuweka saini mikataba mbalimbali ikiwemo ile inayohusu huduma za kijamii, zimechangia kuharakisha maendeleo.


Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Celina Kombani, aliyasema hayo Bungeni mjini Dodoma mwishoni mwa wiki wkati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mtoni Zanzibar, Bw. Faki Haki Makame (CUF).

Katika maswali yake yenye sehemu mbili, Bw. Makame alitaka kujua Serikali inaposaini mikataba hasa inayohusu miradi ya huduma za jamii inazingatia vipi gharama za huduma hizo kwa wananchi wenye uwezo mdogo kifedha.

“Mheshimiwa spika, kabla Serikali haijatia saini mikataba ya uwekezaji ikiwemo ya huduma za jamii, mikataba hiyo hujadiliwa kwanza na kamati ya majadiliano.

“Kamati hii huakikisha vipengele vya mkataba husika, vinazingatia maslahi ya Taifa kama ile inayohusu huduma za jamii hususan maji, afya, simu na reli,” alisemaa Bi. Kombani.

Aliongeza kuwa, kupitia majadiliano hayo kamati huangalia nyanja zote zikiwemo sheria, fedha, uchumi, teknolojia na mazingira.

“Mheshimiwa spika, usimamizi wa kampuni mbalimbali hufanywa na sekta husika kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazohusu sekta hiyo mfano sekta ya madini, Wizara ya Nishati na Madini ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia kwa niaba ya Serikali kama ilivyoainishwa katika sheria namba 14 ya mwaka 2010,” alisema.

No comments:

Post a Comment