14 November 2011

Taasisi za fedha zashauriwa kusaidia elimu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TAASISI  za fedha nchini zimeshauriwa  kusaidia sekta ya elimu nchini kama njia ya kufikia maendeleo ya kweli.

Ushauri huo ulitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipokua akipokea hundi kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) mkoani Kagera.

“Nachukua nafasi hii kuishukuru sana Bank of Afrika tawi la Tanzania kwa msaada wake,”  alisema.

Alisema msaada huo ni hatua muhimu kusaidia ujenzi wa kituo cha chuo hicho mkoani Kagera ambacho kitaanza na fani ya ualimu.

Aliongeza kwamba mchango huo ni muhimu sana kwa wakati huu ambapo Mkoa wa Kagera bado unasuasua kimaendeleo na kielimu ukilinganisha na mikoa mingine nchini.

Meneja Mwendeshaji wa Bank of Africa Tanzania Ammish Owusu-Amoah alisema benki hiyo imeamua kutoa mchango huo kama njia moja wapo ya kushiriki katika kuchangia maendeleo ya nchi kutokana na faida wanayoipata.

“Tutaendelea kusaidia sekta ya elimu nchini,” alisema Mkurugenzi huyo wakati wa kukabidhi hundi zenye jumla ya shilingi milioni kumi kwa SAUT na shule ya sekondari ya Mt. Maria Goret iliyopo katika manispaa ya Moshi.

Benki hiyo imetoa jumla ya sh. milioni kumi kwa taasisi hizo mbili za elimu, kila moja ikipokea shilingi milioni tano.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya Mt. Maria Goret, Bw. Willbard Kassian alitoa shukrani zake kwa benki hiyo kwa kusaidia sekta ya elimu nchini.

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa uamuzi wenu wa kuchagua shule yetu na kuipatia msaada huu,” alisema.

Alisema fedha hizo zitasaidia katika ununuzi wa basi la wanafunzi.

2
Kampuni ya kukusanya ushuru yalia na TATO
Na Richard Konga
Arusha

KAMPUNI ya kukusanya ushuru wa magari  ya watalii katika Halmashauri ya Manispaa ya Arusha  Kilimanjaro Millenium Printers Ltd(KPML) imeshindwa  kukusanya ushuru huo  baada madereva wa magari hao  kugoma kuliba ushuru huo.

Taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa kampuni hiyo,Bw. Thomas Munisi kwa waandishi
wa habari ilieleza  kuwa kampuni yao imekuwa ikikabiliwa na changamoto katika ukusanyaji wa ushuru kwa magari  ya watalii baada ya uongozi wa Chama cha Waendesha Watalii (TATO) kuwazuia wanachama wake.


Alisema kuwa pamoja na kampuni yao kufanya jitihada za mara kwa mara za kuuandikia barua uongozi wa chama hicho juu ya hatua hiyo lakini chama hicho kimeshindwa kutoa ushirikiano hadi sasa.

Bw. Munisi alisema kuwa  Halmashauri ya Jiji la Arusha nayo imeshindwa kufikia malengo ya
kukusanya mapato yake ya ndani kutokana na changamoto hiyo huku akiziomba mamlaka husika kuingilia kati na kutatua hali hiyo.

Akizungumzia  kuhusu madai hayo
Katibu wa chama hicho,Bw. Mustapha Akonaay alisema kwamba chama chao hakikubaliani
na ukusanyaji wa ushuru kwa magari ya wanachama wao kwa kuwa wao hawaegeshi
magari yao katika vituo vya mabasi bali katika ofisi mbalimbali za utalii
jijini hapa.

Pamoja na kukiri kupokea
barua ya maelekezo kutoka kampuni ya ukusanyaji wa ushuru huo katibu huyo
alidai kuwa hata hivyo kampuni hiyo haikustahili kuwaandikia wao barua hiyo bali
uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha huku akisema kuwa wamejipanga  kupinga
ukusanyaji wa ushuru huo kwa
kufikisha madai yao mahakamani.

Naye,Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha,Bw. Estomihn Chang'ah  alipohojiwa juu ya sakata hilo,alidai kwamba kampuni za utalii zimekuwa zikivunja sheria
inayowataka kulipa ushuru wa magari yao kwa wakala aliyepitishwa na halmashauri.

"Hizi kampuni za utalii muda mrefu zimepewa  taarifa za kulipia magari yao lakini yamekuwa
yakikaidi ila tunayaagiza yalipe ushuru kwa wakala bila usumbufu na tupo tayari
kuchukua hatua iwapo wataendelea kukaidi," alisema

3
SACCOS waomba kuondolewa kodi
Na Rehema Maigala

VIONGOZI wa SACCOS  Mkoa wa Dar es Salaam wanaiomba Serikali kuwaondolea suala la ulipaji wa kodi ili wazidi kuwahudumia Watanzania hasa wale wenye kipato cha chini.

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja wamajadiliano juu ya ulipaji wa kodi katika SACCOS  uliofanyika jana jijini Dar es Salaam viongozi hao walisema kuwa SACCOS  nyingi zinaweza kupoteza muelekeo na hata kufa kabisa kwa sababu ya ulipaji wa kodi

Mwakilishi wa wanachama wa SACCOS alisema zipo baadhi ya SACCOS  bado ni changa hivyo kulipa asilimia 30  zinaweza kupoteza muelekeo wake wa kiutendaji.

"Tunapenda kuwahudumia Watanzania wale wenye vipato vya chini sasa ikiwa Serikali itatutoza pesa nyingi hivyo tutawezaje kuendesha hizi SACCOS," alisema

Alisema wateja wao wakubwa ni wafanyabiashara wadogowadogo ambao wengi wao hawachukui mikopo mikubwa kwa sababu ya biashara zao bado hazijakuwa.

Naye,Mwenyekiti wa SACCOS  ya Kitunda Bw.Elias Lawe,alisema kuwa viongozi wote wa SACCOS  Tanzania washirikiane kwa pamoja kulipinga suala la ulipaji wa kodi wa asilimia 30 la sivyo itasababisha SACCOS  nyingi kupoteza muelekeao wake.

Alisema kuwa Serikali ifikiri na ijiulize kuwa SACCOS  zinaendeshwaje ndipo waanze kutoza ushuru.

No comments:

Post a Comment