04 November 2011

Chad yaiendea Stars Tunisia

Na Zahoro Mlanzi

WAPINZANI wa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za mchujo wa kuwania kucheza hatua za awali za Kombe la Dunia, timu ya Chad imepiga kambi nchini Tunisia kujiandaa na mchezo dhidi ya Taifa Stars utakaopigwa Novemba 11, mwaka huu.


Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhiwa vifaa vya michezo vya timu ya taifa kutoka kwa wadhamini Benki ya NMB, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema Chad imejificha Tunisia na wapo huko tangu wiki mbili zilizopita.

Alisema timu hiyo inaonekana kuipania Taifa Stars na ndio maana wameanza kambi mapema kwa wachezaji wa wanaocheza ligi ya ndani na wale wa kulipwa watajiunga siku chache kabla ya kucheza na Stars.

"Chad ni timu ngumu sana licha ya kwamba watu wengi wanaweza kuidharau lakini wameamua kuuchukulia kwa umakini mkubwa mchezo huu na ndio maana wakaahirisha shughuli zao zote na kuweka kambi mapema nchini Tunisia," alisema Osiah.

Alisema timu hiyo ina mshambuliaji (hakutaja jina) ana umrefu wa zaidi ya mita 1.8 ambaye ndiye wanaomtegemea pamoja na wengine wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.

Wakati huohuo, Benki ya NMB, imetoa vifaa vya michezo kwa timu hiyo vyenye thamani ya sh. milioni 9 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Mkurugenzi wa Masoko wa benki hiyo, Iman Kajura alivitaja vifaa hivyo ni viatu na mabegi jozi 30, jezi jozi mbili, nguo za mazoezi jozi 54 na za ofisa wa timu jozi 14, grovu tatu na tracksuit 30.

Alisema anajua Taifa Stars ipo vitani na siku zote vita inahitaji vifaa na kujiandaa ili uweze kupambana vizuri na ndio maana wameamua kutoa vifaa hivyo ili ijiandae na mapambano.

Ciao

2 comments:

  1. Osiah kazi yako ni kuwasifia Chad,Je na sisi tumejiyarishaje?.Kila siku matayarisho yetu ni mabovu alafu tunataka tushinde kivipi?
    Wenzetu wamepiga kambi tena wiki mbili zilizo pita na tena kwenye nchi yenye jina kubwa kisoka siui sisi labda tuta tafuta mechi na Palestina au jordan alafu baada ya mchezo wapenzi wanaanza kumlaumu kocha.

    ReplyDelete
  2. Babu hana jipya. Ligi inaendelea jamaa kajichimbia Denmark, akirudi anaita mafaza kwenye timu. Tujiandae kuendelea kulaumiana.

    ReplyDelete