04 November 2011

Mosha atimiza ahadi yake Yanga

Awamwagia wachezaji 'mahela


Na Mwandishi Wetu


MAKAMU Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Davis Mosha ametimiza ahadi yake kwa wachezaji wa timu hiyo baada ya jana kuwakabidhi sh. milioni kumi ikiwa ni furaha kwake kutokana kuwafunga wapinzani wao, Simba bao 1-0 katika mechi ya kumalizia mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.


Mechi hiyo ilipigwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mosha alitoa ahadi hiyo, mara baada ya ushindi huo akiwa nchini Australia, alipokwenda katika biashara zake.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwa niaba ya Mosha, Abel Mcharo alisema fedha hizo ni ahadi ya kiongozi huyo wa zamani wa Yanga, ambayo aliahidi baada ya ushindi huo kupatikana.

Alisema Mosha amesikitika mno kuiokosa mechi hiyo, na hiyo ilisababishwa na yeye kuwa safari nje ya nchi kikazi.

Mcharo alisema, Mosha amewataka wanachama wa Yanga kushikamana na kuangalia wanapokwenda, wasiangalie walipotoka kwa kuwa umoja unahitaji kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kitu chochote.

Alisema kutolewa kwa fedha hizo, si kwa faida ya Mosha, bali ni kwa wana-Yanga wote hivyo amewataka kuwa kitu kimoja kwa kuinga mkono timu yao.

Akipokea fedha kwa niaba ya wachezaji, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic alimshukuru Mosha kwa fedha hizo na kusema kuwa itakuwa ni motisha nzuri kwa wachezaji kuongeza ari.

"Hatua hii ya Mosha inapaswa kuigwa na mashabiki na wwanachama wa Yanga, kwa kuwa kufanya hivi itasaidia kuwapa ari wachezaji ili waweze kufanya vizuri zaidi," alisema Papic.

No comments:

Post a Comment