29 November 2011

Bab atua Azam FC

Na Mwandishi Wetu

Baada ya mkataba wake kusitishwa na Klabu ya DT Long An ya Vietnam, kiungo Abdi Kassim 'Babi' jana amesajili kuichezea Azam FC ya
Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa alisema Babi amesajili kwa mkataba wa miezi 18, sawa na mwaka mmoja na nusu akiwa mchezaji huru.

Babi amekuwa mmoja wa wachezaji waliosajiliwa na klabu hiyo katika kipindi cha dirisha dogo la usajili, pamoja na mchezaji Kipre Bolou Michael kutoka Ivory Coast.

Michael amejiunga na Azam FC kwa mkataba wa mwaka mmoja utakaokamilika Novemba mwaka 2012 ni pacha wa mshambuliaji wa klabu hiyo, Kipre Tchetche.

Akizungumzia gaghama za usajili kwa wachezaji hao alisema ni makubaliano kati ya mchezaji na klabu na ni siri, kutokana na sehemu ya mikataba inayoainishi usiri wa taarifa za mchezaji, ikiwemo gharama za usajili.

Idrissa aliongeza kuwa wachezaji hao, wataungana na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba aliyetoka Moro United.

Babi ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, alijiunga na DT Long An Januari mwaka huu akitokea Yanga ya Dar es Salaam.

Mkataba wake na klabu hiyo, umesitishwa baada ya Long An kushuka daraja msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment