29 November 2011

Kili Stars kibaruani tena leo

Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA watetezi wa michuano ya Chalenji Kilimanjaro Stars, leo itakuwa na kibarua kingine ambapo itamenyana na Djibouti, katika
mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kabla ya mechi hiyo kuanza, kwenye uwanja huo itatanguliwa na mechi kati ya Rwanda 'Amavubi' na Zimbabwe, itakayoanza saa nane za mchana.

Mchezo huo ni muhimu kwa Kili Stars, ambayo ndiyo timu mwenyeji wa mashindano hayo kuweza kuibuka na ushindi, ili ifufue matumaini ya maelfu ya Watanzania ambao wapo nyuma yao, hasa ikizingatiwa mechi ya kwanza walipoteza.

Kili Stars ilifungua mashindano hayo kwa kuumana na Amavubi, katika mchezo uliokuwa na ushindani, lakini mpaka kipyenga cha mwisho kikipulizwa Kili Stars ililala kwa bao 1-0.

Baada ya matokeo hayo, yalizungumzwa mengi huku wengine kuhoji uwezo wa baadhi ya wachezaji, walioitwa katika kikosi hicho na wapo waliowashushia lawama makocha, Charles Boniface Mkwassa na Jamhuri Kihwelu 'Julio' kwa kupanga kikosi dhaifu.

Lakini pamoja na lawama hizo, Mkwassa alizungumzia kikosi chake ambapo alisema haikuwa na maandalizi ya kutosha kujiandaa na michuano hiyo, pamoja na kukosa mechi za kirafiki.

Alisema kutokana na hilo hakupata muda wa kuwaona wachezaji wake zaidi ya mazoezini, hivyo ana imani kadri wanavyocheza mechi ndivyo watakavyobadilika na kucheza, kama Watanzania wanavyopenda timu hiyo icheze kwa kuibuka na ushindi.

Kili Stars ipo Kundi A, pamoja na timu zingine za Zimbabwe na Rwanda ambapo ipo katika nafasi ya tatu ikiwa haina pointi sawa na Djibouti ila zinatoafutiana kwa mabao, Zimbabwe ndiyo kinara wa kundi hilo ikifuatiwa na Rwanda.

Katika mchezo wa leo, Kili Stars haina budi kupata ushindi mnono huku ikiiombea mabaya Zimbabwe na Rwanda zitoke sare, ili zifikishe pointi nne na yenyewe iwe na tatu ili kusubiri michezo ya mwisho iamue ni timu zipi, zitatinga robo fainali.

Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, Kili Stars itamaliza mechi yake ya mwisho dhidi ya Zimbabwe na Rwanda itacheza na Djibouti, hivyo kila moja itakuwa imeshikilia tiketi yake ya kusonga mbele.

Nyingine nyingine kwa leo, itakuwa ni kati ya Rwanda na Zimbabwe, ambapo kila moja itataka kuibuka na ushindi ili ijihakikishie nafasi ya kutinga robo fainali.

Timu hizo katika mechi zao za kwanza, zilionesha kandanda zuri ambapo zote zinacheza staili inayofanana kwa kupiga pasi nyingi, huku zikishambulia kwa kushtukiza.

No comments:

Post a Comment