Na Mwajuma Juma, Zanzibar
KAMATI ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar (Mapinduzi Cup), imesikitishwa na timu ya taifa ya Zanzibar
'Zanzibara Heroes' inayoshiriki mashindano ya Chalenji, Dar es Salaam kwa kukumbwa na ukata wa fedha.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mohammed Raza, wakati uzinduzi wake uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi juzi.
Alisema ni aibu kwa timu hiyo kuonekana ikihangaika huku na kule, kutafuta fedha wakati ilifanyika harambee maalumu ya kuisaidia timu hiyo na mamilioni ya fedha ytalikusanywa.
"Nashangaa kuona timu hii, inashiriki mashindano ikiwa katika hali ngumu, wakati ilifanyika harambee iliyoongozwa na Rais wa Zanzibar na fedha nyingi zilikusanywa,” alisema Raza.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja kwa Serikali kuwa makini, wakati wanapoalikwa shughuli kama hizo kwa maandishi ili kujulikana fedha zinazochangishwa zinatumika kwa namna gani.
“Lazima kuwepo na utaratibu maalumu, wakati zinapojitokeza kampuni au taasisi kuchangisha fedha kwa ajili ya timu za taifa au matukio mengine ya kitaifa, lazima hesabu zifanyike,” alisema.
Mapema mwaka huu Kampuni ya Feature Century, ilichangisha fedha kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo ya taifa, ambapo zaidi ya sh. milioni 30 zilikusanywa katika harambee iliyomshirikisha Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.
Katika uzinduzi huo, Balozi Seif alisema serikali itakuwa na ushirikiano wa hali na mali kwa kamati hiyo, ili iweze kufanya kazi kwa pamoja.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi hufanyika kila mwaka, na hushirikisha timu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo bingwa mtetezi wa kombe hilo ni Simba ya Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment