16 August 2011

Watuhumiwa kurudufu CD kuendelea kufikishwa kortini

Na Stella Aron

JESHI la Polisi limesema litaendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanaodaiwa kurudufu CD za wasanii bila ya idhini yao.Akizungumza na Majira jana
jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni (kipolisi), Charles Kenyela, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutokana na msako unaoendelea kufanywa na Kampuni ya Msama Auction Mart ya jijini Dar es Salaam.

"Kuna baadhi ya watuhumiwa tumewafikisha mahakamani kwa tuhuma za kurudufu CD za wasanii, na huu msako unafanywa na Kampuni ya Msama Auction Mart kwa kushirikiana na polisi, " alisema Kenyela.

Alisema katika msako uliofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita, watuhumiwa zaidi ya watano wamefikishwa mahakamani na bado msako huo unaendelea ili kupunguza kilio cha wasanii kuibwa mali zao.

Hata hivyo, Kenyela alisema kuna watuhumiwa wengine wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa upelelezi.

Katika operesheni hiyo, kampuni hiyo imefanikiwa kukamata mitambo ya kurudufia CD za wasanii hao maeneo ya Mabibo, Ubungo na Kinondoni.

Kamanda Kenyela alisema mpango huo wa kuwakamata wezi wa CD za wasanii utaendelea kwa kushirikiana na Kampuni ya Msama Auction Mart.

"Lengo letu ni kuhakikisha wizi wa kurudufu CD za wasanii unakwisha, hivyo tutaendelea kushirikiana Msama mpaka tufikie malengo yetu," alisema.

No comments:

Post a Comment