16 August 2011

Mikoa 14 yathibitisha kushiriki Rock City Marathon 2011

Na Mwandishi Wetu

MIKOA mitano zaidi imethibitisha kushiriki  mashindano ya Rock City Marathon 2011 yatakofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Septemba 4, mwaka
huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa mashindano hayo, Zaituni Ituja wa Kampuni ya Capital-Plus International (CPI) inayoandaa mashindano hayo, alisema wanariadha wengine wa mikoa mitano wamejitokeza kushirki mashindano hayo.

Zaituni aliitaja mikoa hiyo ni Ruvuma, Dodoma, Kilimanjaro, Rukwa na Mbeya.

Mikoa mingine iliyothibitisha kushiriki mashindano hayo ni Dar es Salaam, Mara, Kagera, Singida, Shinyanga, Arusha, Manyara, Tabora na mwenyeji Mwanza.

Mashindano hayo yameungwa mkono na Chama cha Riadha Tanzania (AT) na Chama cha Riadha cha Mkoa wa Mwanza.

"Ni faraja kwetu kuona washikiri wengi zaidi wanajitokeza katika mashindano ya mwaka huu ukilinganisha na miaka iliyopita. Hii inathibitisha kukua kwa mashindano mwaka hadi mwaka, na ushindani utakuwa mkubwa zaidi," alisema.

Kampuni ya CPI ya Dar es Salaam inaandaa mashindano hayo kwa mara ya tatu, ambapo mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2009.

Mbio hizo zitaanzia Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na kuelekea njia tofauti za Jiji la Mwanza na kumalizikia katika uwanja huo.       

Alisema mashindano ya mwaka huu yamedhaminiwa na Geita Gold Mine, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), New Africa Hotel, Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Bank M.

Wengine ni MOIL, New Mwanza Hotel, Shirika la Hifadhi ya Wanyapori Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).  

Zaituni alisema mbio mbali ya ndefu, pia kutakuwa na mbio za kilomita tano kwa wote, kilomita tatu kwa  wazee wa kati ya umri wa miaka 55 na zaidi, mbio za  kilomita tatu kwa watu wenye ulemavu na mbio za kilomita mbili kwa watoto wenye miaka  kati ya 7-10.     

Alisema fedha zitakazopatikana kutokana na fomu za usajili,  zitakwenda katika mfuko wa kuwasaidia watu wenye ulemavu mkoani Mwanza.       

Fomu za kujisajili zinapatikana Ofisi za Uwanja wa CCM Kirumba, Capital- Plus International Limited- DSM, Makao Makuu ya Chama cha Riadha Tanzania (RT) jijini Dar es Salaam na Ofisi za MRAA Mwanza.

Pia, zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com au info@capitalplus.co.tz.


No comments:

Post a Comment