Na Mwandishi Wetu
WASHIRIKI 30 wa Vodacom Miss Tanzania waliokuwa kwenye ziara ya kimafunzo mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Arusha, wamemaliza ziara na kurejea ndani ya
jumba lao Vodacom House 'Vodacom House'.
Ziara hiyo ya mafunzo iliwachukua siku 10, iliwafikisha wanyange hao kwenye Hifadhi za Taifa za Mikumi, Ngorongoro, Tarangire na shule ya wasichana ya Maasai iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, alisema maeneo mengine waliyotembelea kujifunza mambo mbalimbali ni shule ya watoto wa kimaasai Monduli, kaburi la hayati Moringe Sokoine, kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), tawi la Arusha na mitambo ya simu ya Kampuni ya Vodacom, ambao ni wadhamini wakuu wa shindano hilo.
Nkurlu alisema warembo hao walijifunza mambo mengi, hasa ya utalii wa ndani.
"Tumemaliza salama ziara hii ya mafunzo, warembo wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo historia na rasilimali zilizopo nchini, utalii, wanyama pori na binadamu wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi za taifa," alisema.
Naye, Mkurugenzi wa kampuni ya Lino Agency, waandaaji wa mashindano hayo, Hashim Lundenga, alisema wanyange hao baada ya kuwasili mjini Dar es Salaam, walipata fursa ya kukutana na ndugu, jamaa na marafiki katika siku ya familia iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania.
"Baada ya ziara ndefu ya Morogoro na kanda ya kaskazini, warembo wamekutana na jamaa zao kwa mazungumzo, kabla hawajaingia hatua ya mwisho ya kumtafuta mshindi. Ni matarajio yetu wataitumia elimu waliyoipata kuvitangaza vema vivutio vya utalii vilivyopo nchini huko waendako," alisema Lundenga.
Mwaka huu warembo waliingia kambini kwa mfumo tofauti na uliozoeleka, kwani wanaishi kwenye jumba maalumu la Vodacom, ambapo matukio yao yatakuwa yakioneshwa kupitia kituo cha televisheni cha Star Tv na Clouds.
Alisema watazamaji watapata fursa ya kupiga kura kumchagua mrembo watakayemwona anafaa.
No comments:
Post a Comment