22 August 2011

Basi la shukurani laua,kujeruhi tisa

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

DEREVA wa basi la Kampuni ya Shukurani,Bw. Shabil Khan (40) amefariki dunia papo hapo, baada ya basi alilokuwa akiendesha kugonga tela la lori eneo la Mbande
wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Katika ajali hiyo, abiria tisa walijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu.

Mashuhuda wa ajali hiyo iliyotokea jana saa 2.15 asubuhi katika eneo la Mbande wilayani Kongwa walieleza kuwa  ajali hiyo ilihusisha basi namba T 494 AAG lilokuwa likitokea Dodoma kwenda  Dar es Salaam, ambapo liligonga tela la lori lenye namba za usajili T 704 ARB baada ya lori hilo kutaka kumkwepa mpanda baiskeli na hatimaye tela  hilo
kuangaka.

Walisema,wakati dereva huyo wa roli akiendelea na juhudi za kumkwepa mpanda baiskeli na tela kuanguka basi  la Shukrani lililokuwa likitokea mjini Dodoma lilijigonga  kwenye trela la lori na kusababisha kifo hicho cha mtu mmoja ambaye ni dereva wa basi la
Shukurani.

Hata hivyo majeruhi wote waliotokana na ajali hiyo walikimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupatiwa huduma  ambapo wengine miongoni mwa majeruhi hao tisa walitibiwa na kuruhusiwa.

Akizungumzia hali ya majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Nassoro Mzee, alisema walipokea majeruhi tisa, ambapo watatu kati ya hao walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Aliwataja waliolazwa katika hospitali hiyo kuwa ni Bw.Alphonce Andrew, Bw.Yaha Omar,Bi. Rahama Salum, Bw.Abduazizi Hirali, Bw.Seleman Said na Bw.Christopher Lazaro.

Alisema majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kupata matibabu ya awali katika hospitali hiyo.

Hata hivyo juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Bw.Stephen Zelothe, kuthibitisha tukio hilo hazikuzaa matunda.

Katika tukio jingine, watu wawili akiwemo mke wa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida,Dkt. Antiphas Swai, wamekufa baada  gari walilokuwa wakisafiria kupinduka baada ya kupasuka kwa tairi la nyuma upande wa kulia.

Wanawake hao waliopoteza maisha walitambulika kuwa ni mfanyakazi Hospitali ya Wilaya ya Manyoni,Bi Suzana Kakwesi, ambaye ni mke wa Dkt. Swai na muuguzi hospitali hiyo,Bi Oliva Mushumbushi.

No comments:

Post a Comment