Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WACHEZAJI wawili wa timu ya soka ya Maili Moja United ya Kibaha mkoani Pwani, wamekwenda kufanya majaribio kwenye timu ya Tigers ya nchini Namibia.Timu hiyo
ya Tiger inashiriki Ligi Kuu nchini Namibia.
Akizungumza na gazeti hili jana mjini Kibaha, Msemaji wa timu hiyo, John Gagarini, alisema mipango ya wachezaji hao kwenda kufanya majaribio, imekamilika.
Gagarini aliwataja wachezaji watakaoondoka wiki hii ni Novat Lufunga ambaye ni beki wa kati na Valentine Kikuo anayemudu nafasi ya ushambuliaji.
"Tumedhamiria kuhakikisha timu yetu inakuwa na mfumo wa kisasa wa kuuza wachezaji nje ya nchi ili waweze kuonesha vipaji vyao, na siyo kuishia nchini, tutaweka utaratibu wa kuwapeleka sehemu mbalimbali ili kuwaongezea uzoefu na baadaye waweze kuichezea timu ya Taifa 'Taifa Stars'" alisema.
Gagarini alisema kuwa, wachezaji hao walipata nafasi hiyo baada ya kocha wao, Lubigisa Lubigisa, ambaye anachezea timu ya Tigers kutakiwa kupeleka wachezaji kwenye timu hiyo na nakala za mkataba wa wachezaji hao zilitumwa wiki iliyopita.
Kwa upande wake Lubigisa, alisema tangu aanze kufundisha timu hiyo, aliona uwezo wa wachezaji hao na kuridhika na viwango vyao.
"Niliwapa kipaumbele wachezaji hao, ni wachezaji wenye uwezo na nidhamu, wanajituma na ninaamini Tigers imepata wachezaji wazuri watakaofanya mambo makubwa," alisema Lubigisa.
Lubigisa alisema anaamini kuwa, wachezaji hao watafuzu majaribio na kuweza kuichezea timu hiyo, akiamini kuwa, wachezaji wa Tanzania wana uwezo mkubwa wa kucheza soka nje ya nchi, lakini tatizo lao kubwa ni kutothamini kinachowapeleka huko na kujikuta wakirudi baada ya muda mfupi.
No comments:
Post a Comment