Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeipongezi timu ya Taifa ya gofu ya wanawake ya Tanzania 'Tanzanite Stars', kwa kutwaa ubingwa wa
Kombe la Challenge kwa wanawake katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Mashindano hayo yalianza Agosti 16 hadi Agosti 18, mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando, alisema chama hicho kimekunwa na mafanikio hayo na kinatoa pongezi za dhati kwa timu hiyo kuweza kutetea ubingwa wake katika mashindano ambayo yanafanyika kila baada ya miaka miwili ambapo yalikuwa ya pili na ya viwanja 54.
Mhando alisema kikosi hicho kinastahili pongezi kwani nchi zote nne zilizoshiriki mashindano hayo ziko katika kiwango cha juu.
Alizitaja timu hizo ni Kenya, Uganda, Zambia na wenyeji Tanzania.
Nchi za Rwanda, Burundi, Malawi, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), zilishindwa kushiriki, lakini tatizo kubwa ni kukosa timu za wanawake.
Tanzania ambao walikuwa mabingwa watetezi wa Kombe hilo ambalo kwa mara ya kwanza walilitwaa mwaka 2009, mjini Kampala, Uganda.
Katibu huyo alisema kikosi hicho cha Tanzaniani kilifanikiwa kutetea ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Alisema hayo ni mafanikio makubwa katika uongozi mpya wa Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) chini ya Rais, Mbonile Burton, tangu kuingia madarakani Juni mwaka jana.
Alisema mafanikio hayo yanafuatia yale ya kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Afrika ya gofu kwa wanawake yaliyofanyika nchini Abuja, Nigeria, mwaka jana.
Mhando alisema TLGU imeweza kutangaza vema gofu ya wanawake na kuweka historia ya kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa kwa mara ya kwanza.
Mwaka huu Tanzania wameibuka mabingwa kwa kishindo zaidi, wakiwaacha wapinzani wao Zambia walioshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mikwaju (strokes) 31.
Mwaka 2009, Tanzania wakiwa ugenini, walishinda kwa tofauti ya mikwaju 20.
"Tunaomba wachezaji wa Tanzanite Stars wakiongozwa na nahodha Madina Iddi, Ayne Magombe, Angel Eaton na Hawa Wanyeche waone mafanikio haya waliyoyapata ni ya watanzania wote, tunayajali," alisema.
No comments:
Post a Comment