16 August 2011

Spika amwekea kinga Pinda

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Bi Anne Makinda amewaonya wabunge na mawaziri kuacha tabia ya kumsumbua Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda anapokuwa ndani ya bunge na
badala yake watumie fursa hiyo ofisini kwake.

Hayo aliyasema jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, akisema suala hilo limekuwa kero kwa Waziri Mkuu kuzongwa zongwa na baadhi ya wabunge na hata mawaziri kwa lengo la kutaka mazungumzo naye ndani ya ukumbi.

Spika alisema kuwa hivi sasa Waziri Mkuu amekuwa akitumia muda mwingi kufanya mazungumzu na baadhi ya wabunge ambao wamekua wakitoka katika viti vyao na kumfuata alipoketi hali ambayo inamfanya Waziri Mkuu ashindwe kufuatilia mambo mbalimbali yanayoendelea bungeni.

“Waheshimiwa wabunge na hata mawaziri na manaibu waziri hali hii inayojitokeza hivi sasa kwa Waziri Mkuu kukosa hata muda wa kusikiliza mambo mbalimbali ndani ya bunge letu kwa kumzonga zonga kwa mazungumzo kama mnaona mnamhitaji zaidi kwa mazungumzo basi akae ofisini kwake, haina sababu Waziri Mkuu kuja bungeni, kwa kuwa inaonekana anakuja kuwasikiliza wabunge tu badala ya kufuatilia mambo mbalimbali yanayohusu bunge,” alisema.

Kutokana na hali hiyo aliwataka wabunge hao kujenga tabia ya kwenda ofisini kwa Waziri Mkuu na kufanya mazungumzo naye huku ndiko mahali ambapo kunastahili.

Alisema kuwa kwanza anasikitika sana kuona mbunge anakuwa na mazungumzo marefu na Waziri Mkuu ambayo yanaweza kuchukua hata dakika 15, hali ambayo alisema kuwa kiongozi huyo hawezi kusikiliza vitu vingine ambavyo vinakuwa vikiendelea ndani ya bunge hilo.

Alisema kuwa tabia hiyo inapaswa kuachwa mara moja na wabunge hao pamoja na mawaziri ili kumpa fursa Waziri Mkuu kufuatilia mambo yanayoendelea ndani ya bunge hilo hasa akiwa na dhamana ya Kiongozi wa Serikali Bungeni.

Hivi karibuni baadhi ya wabunge walighushi saini ya Bw. Pinda katika ujumbe uliotumwa kwa wenzao, ukionesha Waziri Mkuu alikuwa anawaita, na walipokwenda kumsikiliza ilibainika kuwa haikuwa kweli.

2 comments:

  1. Kwani kazi ya Waziri Mkuu ni nini kama sio kujibu maswali - hasa yale yanayohusi uzembe na utendaji mbovu wa serikali yake. Wee mama vipi?

    ReplyDelete
  2. Ni vema kutafuta busara na msimamo wa waziri mkuu mapema kuliko kungoja mpaka mambo yaharibike kama ya Ngeleja. Kujiamini ni vizuri lakini isiwe zaidi ya busara mtu aliyopewa na mwenyezi mungu. Hivyo kuuliza kwa mkubwa wako ni kujiongezea imani.

    ReplyDelete