16 August 2011

Polisi kushtakiwa kwa kutorosha mahabusu

Na Stella Aron

JESHI la Polisi limesema kuwa limeandaa utaratibu wa kuwashtaki kijeshi askari wake wanne wa Kituo cha Magomeni kwa tuhuma za kusababisha mahabusu 13 kutoroka katika
kituo hicho.

Mahabusu hao waliachwa pekee bila ulinzi huku wakiwa na ndugu zao ambao waliwapeleka chakula, walitoroka Agosti 9, mwaka huu usiku baada ya umeme kukatika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Bw. Charles Kenyela alisema katika uchunguzi umebaini kuwa kutoroka kwa mahabusu hao kunatokana na uzembe wa polisi hao.

Kamanda Kenyela alisema ili kukomesha tabia hiyo jeshi hilo linatarajia kuwashtaki katika mahakama ya kijeshi polisi hao ili iwe fundisho wa polisi wengine.

"Hawa mahabusu walitoroka baada ya kuachwa na ndugu zao waliofika kwa ajili ya kuwapa chakula ambapo polisi walipaswa kukaa nao na kuimarisha ulinzi," alisema Kenyela.

Alisema kutokana na kukatika kwa umeme ghafla kituoni hapo mahabusu hao walipata nafasi ya kutoroka na kusababisha ugumu wa polisi kuwatafuta.

Aliwataja waliotoroka kuwa ni Bw. Abdallah Saidi (29), mkazi wa Manzese, Bw. Bakari Athumani (Mburahati), Bw. Omary Hamad (Mburahati), Bw.Rebefu Annastozuis (Magomeni).

Wengine ni Bw. Abdallah Masudi (Magomeni), Bw. Wakati Hudja  (Tandale), Usigali David (Tegeta), Bw.Abdallah Salumu (Manzese), Bw.Hemed Athuman (Magomeni).

Wengine ni  Bw.Jumanne Tawaya (Magomeni), Bw. Matuguli William (Kigogo), Bw. Edward Maleko (Magomeni) na Bw.Magali Hassa (Magomeni).

Alisema kati ya mahabusu hao, Bw. Wakati Hudja (23) ndiye aliyekamatwa na wengine wanaendekea kutafutwa.

2 comments:

  1. Polisi wakiambiwa wao ni jeshi la majambazi wanakana wakati uchafu wao wote umedhihirika.
    Kuua watu wasio na hatia (kama wale vijana wa mahengi); kuficha na kuwalinda baadhi ya wahusika katika mauaji (vijana wa Mahenge tena; kutumia au kukodisha silaha za jeshi kwa shughuli za ujambazi; kula rushwa kwa ulafi mkubwa, kuwa na vitambi vikubwa hadi kushindwa kufanya kazi; kubambikia watu kesi, n.k.

    ReplyDelete
  2. Pamoja na madhambi makubwa waliyonayo polisi kwa kupenda kupewa hongo hata kwa jambo lililowazi; katika hili mimi nadhani TANESCO nayo inapaswa kuwajibika. Hata kama wangekuwa karibu sio rahisi kukabiliana na muhalifu sugu katika giza. Labda kwa kuwa ni wapenda hongo inawezekana umeme kilikuwa ni kisingizio tu. Walishapewa kitu kidogo nao wakasema umeme ukikatika (kwa kuwa ratiba inajulikana) anzeni mbele sisi tutajua jinsi ya kujitetea.

    ReplyDelete