16 August 2011

Rais Mubarak afikishwa tena kizimbani

Rais Mubarak wa Misri

CAIRO,Misri

KESI ya aliyekuwa kiongozi wa Misri,Bw. Hosni Mubarak, iliendelea kuunguruma jana
mjini Cairo ikiwa ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kufikishwa mahakamani hapo.

Bw.Mubarak, 83,alifikishwa mahakamani hapo akiwa amebebwa kwenye kitanda cha kubebea wagonjwa, huku akizungumza na wanaye Bw. Alaa na Bw Gamal ambao nao wanatuhumiwa kwa ufisadi.

Kiongozi huyo ambaye aliondolewa madarakani kwa nguvu ya umma mwezi Februari mwaka huu anakabiliwa na adhabu ya kifo endapo atatiwa hatiani.

Habari kutoka nchini humo zilieleza kuwa mamia ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia walikuwa wametanda nje ya mahakama wakati kesi hiyo ikisikilizwa mapema jana.
Ilielezwa kuwa wakati kesi hiyo ikiendelea mamia ya wafuasi wa kiongozi huyo pia, walikuwa wamekusanyika nje ya mahakama hiyo wakiimba kuwa Rais Mubarak ataendelea kuwa raia wa Misri hadi hapo atakapofariki huku wengine wakisema kuwa kiongozi huyo siyo sawa na rais wa zamani wa Irak, Bw. Sadam Hussein.

Ndani ya mahakama, Jaji Ahmed Refaat aliuliza kama kulikuwepo na utetezi upande  Bw. Mubarak,na kisha kufuatia wanaye wawili wa kiume.

Hata hivyo wakati wa kesi hiyo kusikilizwa kwa mara ya kwanza Jaji alijikuta katika wakati mgumu katika kutoa maelekezo, baada ya kubainika kuwa walikuwepo mawakili zaidi ya 100 kutoka pande zote mbili,hivyo jana akaanza  kuchunguza kila ushahidi uliofikishwa mbele yake kabla ya kuomba mapumziko.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC,Bi.Yolande Knell alisema kuwa wanasheria  wa familia ya waandamanaji waliouawa katika ghasia tayari wameshauliza  kwa ajili ya kupata  kumbukumbu zaidi kama kulikuwepo mawasiliano kati ya Bw.Mubarak na maofisa wake.

Mwandishi huyo wa BBC, alisema kuwa familia zinataka kufahamu agizo lililotolewa na kiongozi huyo kwa maofisa wake wakati polisi wakijaribu kuzuia ghasia kama alitoa amri ya kutumika njia za kikatili.

Mawakili hao wa utetezi wanadai kuwa  kiongozi wa kijeshi, Bw.Mohamed Hussein Tantawi, anayeongoza halmashauri ya kijeshi ambayo alichukua madaraka kutoka kwa Bw. Mubarak lakini ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi  kwa miongo miwili, ni lazima atoe ushahidi.

Walisema,ushahidi wake dhidi ya Bw. Mubarak ndiyo unaweza kudhihirisha ukweli.Kwa upande wake wakili wa Bw.Mubarak,Bw. Farid al-Deeb,alimuomba jaji anayesikiliza kesi hiyo kuita mashahidi 1,600 ingawa wachunguzi wa mambo wanadai kuwa idadi hiyo huenda ikapungua.

Bw. Mubarak anaripotiwa kuwa katika hali mbaya kiafya na madaktari wamekuwa wakifuatilia hali yake katika hospitali ya kijeshi iliyopo karibu na mji mkuu  wa Cairo.(BBC).


2 comments:

  1. Marais mafisadi wa Africa nao waanze kuweka maji vichwani mwao wakisubiri nao kunyolewa. Wasione raia wao wamekaa kimya, siku moja yatawatokea puani.

    ReplyDelete
  2. sawa kabisa hasa Mkapa na Kikwete, maraisi mabomu cjapata kuona hasa hasa kikwete ndio bomu namba moja. kaleta udini kupata uongozi. kati ya watu 19mln waliojiandikisha kapata kura 5mln?! jamani na bado watz tuko kimya tunaporwa nchi yetu na mafisadi?

    ReplyDelete