16 August 2011

Rais Mutharika awaangukia wanaharakati

Rais wa Malawi Bingu  wa Mutharika
LILONGWE,Malawi

RAIS wa Malawi,Bw. Bingu wa Mutharika ametoa wito kwa wanaharakati kufutilia mbali maandamano ya
kupinga serikali yaliyopangwa kufanyika Jumatano wiki hii.

Makundi ya kutetea haki za  kiraia yanapanga kile yanachoita makundi ya uangalizi ya kijamii kupinga kile wanachosema ni kushindwa kwa serikali kushughulikia matakwa yao.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa juzi, Rais Mutharika alisema huenda hali Jumatano ikageuka kuwa ya ghasia hivyo akawaomba waandalizi wa maandamano hayo kutafakari upya juu ya hatua hiyo.

Mwezi uliopita  watu 19 waliuawa, baada ya kuzozana na polisi  katika maandamano ya kupinga serikali yaliyofanyika katika miji mitatu mikubwa nchini humo.

Maandamano hayo yamechochewa na ufukara unaokithiri katika kila pembe ya nchi, uhaba wa mafuta na fedha za kigeni.

Rais Mutharika ameapa kuendelea kuwakamata viongozi wa maandamano ya mwezi Julai.

Ijumaa iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza,Bw. William Hague alieleza wasiwasi wake juu ya hali nchini Malawi.

Alimwomba Rais Mutharika kuruhusu mjadala halali wa kidemokrasia na kuzungumza na makundi ya kutetea haki za kiraia.

Uingereza ilisitisha msaada kwa Malawi mapema mwaka huu kufuatia mzozo wa kidplomasia.(VOA).

No comments:

Post a Comment