16 August 2011

EWURA sasa yasimangwa

*Ni kwa kupandisha upya bei ya mafuta
*Yenyewe yasisitiza ni soko la dunia

Na Waandishi Wetu

BAADHI ya wananchi wa kada mbalimbali nchini wameishauri Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuwa makini katika utoaji wa maamuzi yake badala ya
kufanya maamuzi yanayosababisha kuyumbisha maisha na uchumi wa Watanzania.

Maoni ya wananchi hao yametolewa kutokana na mamlaka hiyo wiki iliyopita kuingia kwenye mgogoro mkubwa na wafanyabiashara wa mafuta pale walipowalazimisha kushushwa za mafuta na kuzipandisha tena kabla hazijaanza kufanya kazi katika baadhi ya maeneo kutokana na kukosekana kwa mafuta.

Hatua ya EWURA kupandisha upya bei imepokewa kwa hisia tofauti na wakazi mkoani Rukwa ambako baadhi ya wananchi wamesema mamlaka hiyo haina msimamo, bali imeshinikizwa na  Wafanyabiashara na si kushuka kwa thamni ya shilingi waka kupanda bi ya katika soko la dunia kama ilivyotangazwa na mamlaka hiyo.

Bw. Ismail Lyombe, dereva taksi mjini Sumbawanga alisema kuwa kinachoonekana ni mamalaka hiyo kukosa msimamo na kuongeza kuwa ana hofu kama wananchi wataiamini tena EWURA.

“Sisi hatuna tena imani na EWURA kwa sababu haina msimamo, kwani siku mbili wanatuambia hivi na siku mbili tena watangaza kitu kingine, sasa si bora wangeacha zile zile bei za awali kabla ya wafanyabiashara hawajagoma?” alihoji Bw. Lyombe.

Naye mkazi Mazwi mjini hapa, Bw. Joseph Wenzely alisema kuwa EWURA wanapaswa kuwajibika kwa kuyumbisha uchumi wa nchi kwa muda wote ambao wafanyabiashara wa mafuta waligoma, kwa sababu mamlaka hiyo ilifahamu ni kipi itakifanya kwa muda mfupi baadaye.

“Hapa sio suala kushuka kwa shilingi tu bali wamewaogopa wafanyabiashara, na sijui kwanini watuhangaishe, wananchi tunakosa mafuta na uchumi wa nchi unsimama kwa siku
kadhaa kutokana na mipango yao isiyo makini, hivi hawakuona viashiria vya bei ya mafuta kupanda kama wao walivyosema? mbona muda umekuwa mfupi sana,” alihoji.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa mafuta mkoani Rukwa tofauti na lilipotolewa tangazo la kupunguzwa kwa bei ya mafuta, jana wameonekana kuchangamkia la kupanda kwa bei kwa haraka na kuanza kuzitumia mara moja.

Mfanyabiashara mmoja anayemiliki kituo cha mafuta mjini hapa ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa wao wanafuata maagizo ya mamlaka hiyo.

“Sisi tunaifuata EWURA inasemaje, na ndivyo tulivyofanya. Hatuwezi kuwapinga na kikubwa tunaangalia biashara zetu zinakwendaje katika kupata faida na sio vinginevyo,”
alisema.

Kauli ya Januari Makamba

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Bw. January Makamba (CCM) alisema kwamba kama serikali itashindwa kuweka wazi kanuni zinazotumika kukokotoa bei ya mafuta, wananchi wataendelea kutokuwa na imani juu ya bei hizo mpya.

"Tunachohitaji kwa sasa ni serikali kuweka wazi formula (kanuni) zinazotumiwa kukokotoa bei za mafuta ili wabunge na wananchi waweze kuzijua kwa kuwa kufanya hivyo hapatakuwepo malalamiko kama bei ya mafuta itakuwa inapanda, lakini wakiendelea kukaa kimya maelewano hayatakuwepo ya kuridhisha," alisema Bw. Makamba.

Wasomi nao wanena


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu alisema kwamba serikali inaelekea kusalimu amri kwa wafanyabiashara, hali ambayo inaashiria hatari kwa taifa hasa upande wa kutoa maamuzi.

"Labda serikali haikuwa makini katika upande wa kutoa maamuzi ya awali kwa wafanyabiashara, ndiyo maana walichokifanya kutangaza bei ya mafuta siku chache kabla ya mgogoro na wafanyabiashara, inadhihirisha kwamba imekosa umakini na hivyo maamuzi yake yanaipeleka pabaya hata kusalimu amri," alisema Profesa Baregu.

Alisema kama serikali itashindwa kutoa ufafanuzi kwa jamii juu ya faida zinazopatikana katika biashara ya mafuta hadi kusababisha wafanyabiashara kugoma kutoa huduma, ni wazi kwamba biashara hiyo imetawaliwa na ufisadi mkubwa.

Kwa upande wakem Dkt. Sengondo Mvungi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alishauri EWURA ifutwe kwa sababu 'haina faida kwa Watanzania kwa sababu ndiyo iliyolifikisha taifa katika wakati mhumu wa kukosa mafuta'.

Alisema EWURA ilipaswa kujua wajibu wake kama idara ya serikali ilipaswa kukaa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) kuagiza mafuta yasiyosafishwa na kuwauzia wafanyabiashara nchini.

"EWURA inakaa kwenye komputa kuangalia bei ya mafuta na kupanga bei, matokeo yake Watanzania wanashindwa kuona chombo hicho kinavyoshindwa kuwasaidia na kupandisha mafuta ya taa kwa kisingizio kuwa yanaongeza uchakachuaji," alisema Dkt. Mvungi.

Alisema serikali hii ni legelege kwa sababu imeshindwa kuwasaidia wananchi wake ambao wameingia kwenye kadhia ambayo wasingeweza kuipata endapo EWURA igejipanga kuondoa matatizo ya mafuta.

"Kama kitu huna uwezo nacho usijiweke kimbelembele, lazima kiundwe chombo cha kuchukua nafasi ya UWURA ya kuagiza mafuta na kuwauzia wafanyabiasha, nao wauzie wenye magari," alisema Dkt. Mvungi.

Alisema UWURA iende 'kuzimu' kwa manufaa ya Watanzania kwa sababu imeshindwa kuonesha kuwepo kwake wala manufaa yake kwa Watanzania.

Kauli ya EWURA

EWURA imesema kuwa utaratibu wa kawaida kutangaza bei elekezi kila baada ya wiki mbili, hivyo mabadiliko ya kipindi hiki yasitafsiliwe vinginevyo.

“Huu ni utaratibu kama ambao umekuwa ukifanyika kwa mfululuzo wa miaka mitatu sasa, ila kitu kipya kwa sasa ni kwa kuwa tunatumia fomula mpya ambayo imetoa unafuu zaidi kwa wananchi ikilinganishwa na iliyokuwepo awali...niweke wazi kuwa hatuwaogopi wafanyabiashara katika hili bali tunafanya kazi kwa kufuata taratibu tulizoziweka,” alisema Bw. Haruna Masebu, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA.

Akizungumzia suala la bei kupanda au kushuka kukiwa na akiba ya mafuta katika vituo, alisema kuwa suala la mabadiliko hayo liko kama suala la kodi ambayo huanza kutumika siku inapotangazwa bila kujali akiba iliyopo, hivyo katika hilo upo wakati ambao wafanyabiashara hunufaika na wakati mwingine hupata hasara.

“Suala la akiba liko katika sura mbili, moja bei mpya inamrudishia mtaji aliyewekeza kwenye akiba alizonazo lakini pili bei mpya inatakiwa kumwezesha kuwa na mtaji wa kutosha kuagiza shehena nyingine kwa bei itakayokuwepo kwenye soko wakati anaagiza na endapo bei haitatosha hataweza kuagiza upya na mzunguko wa biashara utakwama na kusababisha mahitaji kutokidhi soko la ndani,” alisema Bw. Masebu.

Alisema kuwa endapo akiba ya mafuta ingekuwa kigezo cha ukokotoaji wa bei, ingebidi kila wakati kuhakiki kwenye maghala na vituo nchi nzima mchakato ambao ni mgumu na si utaratibu wa biashara ya mafuta duniani kote.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na mabadiliko, kanuni mpya inayotumiwa na EWURA kwa sasa imeendelea kutoa unafuu kwa watumiaji ikilinganishwa na kanuni ya zamani kwa kuwa bei za reja reja na jumla zingepanda zaidi.

“Ni dhahiri kuwa kama nchi bado tunapata madhara ya bei za mafuta kutokana na kupanda kwa bei katika Soko la Dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani,” alisema Bw. Masebu.

Katika hatua nyingine, inachunguza mwenendo wa kampuni za Total na Oryx baada ya kudaiwa kuwa baadhi ya vituo vyake haviuzi mafuta na itatoa maamuzi baada ya kujiridhisha.

Bw. Masebu, alisema kuwa mamlaka yake haiwezi ikatoa adhabu kwa kampuni ya mafuta kwa kukurupuka hivyo suala la vituo hivyo bado linalifanyiwa kazi.

Imeandikwa na Godfrey Ismaely, Salim Nyomolelo, Grace Michael na Sammy Kisika

4 comments:

  1. Na kwanini isisimangwe? Hivi Watanzania na wabunge wetu tumekuwa vipofu kiasi kwamba hatuoni huu ulikuwa ni usanii tu wakuwadanganya wabunge waipitishe bajeti iliyokataliwa hapo awali. Punde baada ya bajeti hiyo kupitishwa wasanii wetu walirudisha bei ya mafuta pale pale ilipokuwa. Wananchi na Bunge lao wamefanywa mabaradhuli na hao mafisadi wanaoiendesha nchi yetu. Uongo waliouonyesha katika hili ni tusi kwa taifa; tumefanywa mbumbumbu wa kutupwa. Hata umeme ambao mgao wake tuliambiwa utaboreshwa ni usanii tu. Lengo lilikuwa kuwapumbaza ili bajeri na Nishati na madini ipitishwe.

    ReplyDelete
  2. I despise the rulers who think people are fools and treat them as such. Look, they never really intend to lower fuel prices. This was just a gimmick to have the budget approved by Parliament. Once that was done they went back to the old prices. There was no sincerity at all in lowering fuel prices in the first places. These guys think we are all imbeciles and that they are the only thinking elite. First they they use bribes (using tax payers money) to get the budget approved; when they are caught with their dirty pants down, and the budget is sent back they look for another dirty trick: lowering the price of fuel for a few days, then revert to the old prices. The devils!

    ReplyDelete
  3. Nadhani Ukweli ni kwamba vigogo wengi wana maslahi katika biashara ya mafuta. Huku sio kuwaogopa as such bali ni maslahi. Wako vigogo wengi wenye vituo vya mafuta na wengine hata kwenye makampuni yaingizayo mafuta. La sivyo wamehongwa na makampuni hayo.

    Tatizo la viongozi na wanasiasa kuingia katika biashara matokeo yake ndiyo haya. Hawajali maslahi ya taifa, bali matumbo yao na familia zao tu. Tazama jinsi walivyofunga reli ya Tanga-Arusha ili magari ya mizigo na ya abiria yanayomilikiwa na mafisadi hao yeweze kutumia barabara badala ya reli. Yambo linalotumia gharama nyingi na kuzeesha barabara zetu. Hii pia ni kwa treni zote ziendazo mikoani. Nchi inaendeshwa na mafisi sio watu.

    ReplyDelete
  4. Mkurugenzi Mkuu wa EURA hawezi kuwa makini na majukumu ya Taasisi yake. Yeye kazi kubwa aliyo nayo ni kusafiri nje ya nchi kila kukicha. Inawezekana hata suti anabadilishia katika ndege. Kama hamuamini fanyeni ulizeni kwa mwezi ni siku ngapi yuko kazini? Halafu nauli anazolipiwa na serikali kusafiri na Mashirika ya ndege kama EMIRATES zinamuwezesha kupata bonasi na tiketi za bure za mkewe kusafiria. Ifikie mahali Watendaji Wakuu waulizwe huko nje kila siku kunaleta tija kwa wananchi au wanajilimbikizia maposho. Afadhali miaka 60 ifike astaafu kwa lazima ili atakayemrithi apewe hadidu za rejea tafauti ikiwepo ya kupungua safari za nje.

    ReplyDelete