31 August 2011

NMCP yabainisha mafanikio iliyopata

Na Mwandishi Wetu

MPANGO wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) umesema vyandarua vilivyotolewa wakati wa kampeni ya kitaifa kwa watoto chini ya miaka mitano vilikuwa vya upana
wa futi nne, urefu futi sita na kina futi saba.

Pia NMCP imefafanua kuwa hakuna utafiti wowote uliofanyika kuhusu vitanda vinavyotumiwa na watoto chini ya miaka mitano, kama ilivyoripotiwa kimakosa kwamba ugawaji wa vyandarua kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ulitokana na utafiti uliobaini kwamba watoto hao wanalala kwenye vyandarua vyenye futi mbili kwa mbili, tatu kwa nne na mbili kwa tatu.

Ufafanuzi huo ulitolewa na Ofisa Mawasiliano na Masoko wa Kitengo cha Vyandarua NMCP, Bw. Godfrey Kalagho, kupita taarifa yake aliyoitoa kwa gazeti hili jana.

Bw. Kalogho alikuwa akitolea ufafanuzi moja ya habari zilizoandikwa na gazeti hili jana. Alibainisha kuwa  kampeni ya kugawa vyandarua ilifanyika katika kanda nane na si nne kwa ilivyoripotiwa.

Alisema tangu 2002 ambapo kampeni ya kutumia vyandarua ilianzishwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilianza kutekelezwa Mpango wa Hati Punguzo kwa wajawazito na watoto.

Alisema mpango huo unaendelea kutekelezwa hadi leo. "Mwaka 2008, Wizara iliendesha kampeni ya kugawa vyandarua kwa watoto wote Tanzania bara wenye umri wa miaka chini ya mitano. Katika kampeni hiyo jumla ya vyandarua milioni tisa vilitolewa kwa watoto walengwa," alisema Bw. Kalagho.

Aliongeza kuwa kuanzia mwaka jana, wizara ilianza tena kugawa vyandarua kutokana na maeneo ya malazi, mpango huu unaendelea ambapo kwa Kanda ya Pwani yenye mikoa ya Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani na Tanga, vyandarua vitagawiwa kuanzia Septemba 9 hadi 13.

Alisema kwa Kanda ya Kaskazini mikoa ni Arusha, Kilimanjaro na Manyara) ndiyo itakayokuwa ya mwisho ambayo ugawaji wake utakuwa mwezi Oktoba.

Alisema chimbuko la mpango huo ni Mkataba wa Abuja wa mwaka 2000. Alisema  mwaka huo, viongozi wakuu wa nchi za Afrika waliweka Azimio la kupunguza ugonjwa wa malaria.

Alisema kati ya mbinu zilizowekwa, mmojawapo ni kuhamasisha wananchi kutumia vyandarua vyeye dawa, pamoja na kuwahimiza kufika kwenye vituo vya afya ndani ya saa 24 waonapo dalili za ugonjwa wa malaria pamoja na nyinginezo.

No comments:

Post a Comment