Na John Gagarini, Kibaha
MAKOCHA wa soka wanaotoka mafunzoni, wametakiwa kuwa chini ya walimu wazoefu kabla ya kupewa timu kufundisha ili wapate ujuzi zaidi.Akizungumza mjini hapa jana
Mwenyekiti wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (TAFCA), Emmanuel Yombayomba alisema baadhi ya makocha hao wamekuwa wakikimbilia kufundisha timu bila ya uzoefu.
Yombayomba alisema ili kocha aweze kukomaa kwanza anatakiwa kupikwa na wakongwe kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali.
“Nalishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuweka utaratibu kwa makocha wanaochipukia kuwa chini ya wakongwe kwa muda japo mwaka mmoja, kabla ya kukabidhiwa timu ili wapate mbinu za wakongwe,” alisema Yombayomba.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni kocha wa Maili Moja Kids ya Kibaha, alisema makocha wapya wamekuwa hawana mbinu za kutosha kama walizonazo wakongwe.
“Ili mpira uweze kukua ni lazima misingi ianzie chini, tangu mapema kwa wale wanaotoa mafunzo kwa wachezaji kwani endapo watakosa mbinu za mchezo huo ni dhahiri kiwango cha soka hakitaweza kukua,” alisema Yombayomba.
Aidha alisema wachezaji wa sasa wanakosa vitu vingi ambavyo makocha hao wachanga hawana, jambo ambalo linasababisha wachezaji kutojua wajibu wao wawapo uwanjani na kutochukulia uzito.
No comments:
Post a Comment