CAIRO, Misri
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limehamishia Misri mechi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, kati ya Libya na Msumbiji iliyopangwa kufanyika nchini
Libya kutokana na sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), bodi ya michezo Afrika pia imeagiza mechi ya hiyo kundi C ichezwe bila mashabiki.
Timu hiyo ya taifa ya Libya, mara ya mwisho kucheza mechi ya kufuzu fainali hizo za mwaka 2012, ilikuwa ni dhidi ya Comoro iliyofanyika pia nchini Mali na tangu zianze harakati za kumng'oa madarakani Kanali Moammar Gadhafi, haijawahi kucheza mechi yoyote ya kimataifa.
Licha ya kutochezea nyumbani kwao, Libya imebaki kuwa timu ambayo haijafungwa katika mechi hizo, huku ikiwa imewakaba koo vinara wa kundi hilo Zambia kwa pointi moja baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare mbili.
Kwa sasa nafasi ya Libya kuandaa fainali hizo za Mataifa ya Afrika mwaka 2013, ipo shakani na CAF inajiandaa kujadili mgogoro unaoikabili nchi hiyo katika kikao kitakachokaa Septemba 28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment