Na Rashid Mkwinda, Mbozi
BAADHI ya wakulima wa zao la mpunga kata ya Kamsamba wilayani Mbozi wamekuwa na tabia ya kubadilishana zao hilo na pombe hali inayowafanya waendelee
kuishi katika maisha magumu kila msimu wa mavuno unapowadia.
Wamejikuta wakinunua mchele kutoka kwa wachuuzi kutokana na wao kubadilishana mpunga na bia wakati wa msimu wa mavuno.
Tabia ya kubadilishana pombe na mpunga imekuwa ikifanywa na wakulima hao wakati wa mavuno ambapo wachuuzi hufika mashambani wakiwa na masanduku ya bia na wakulima hushawishika kunywa na kujikuta wakibadilishana mpunga na pombe hizo.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya wauza pombe wakienda na kreti za bia mashambani wakati wa mavuno ambapo wakulima wanapolewa hushawishika kuendelea kunywa na hatimaye hubadilishana bia na debe la mpunga.
Hali hiyo ilianza kuibuka wakati wa mwanzo wa mavuno ya mpunga ambapo debe moja la mpunga lilikuwa likiuzwa kati ya sh. 5,000 hadi sh. 6,000 ilhali chupa moja ya bia ilikuwa ikiuzwa kati ya sh. 1800 hadi sh. 2,000 na hivyo kuwafanya wakulima kunywa chupa kati tatu hadi nne kwa debe moja la mpunga.
Bw. Simchimba alisema kuwa hali hiyo iliwakumba wakulima wengi wa maeneo hayo, hivyo kusababisha kushindwa kuhifadhi chakula na hivyo kusababisha baadhi yao kuanza kununua mchele kwa wachuuzi kati ya mwezi Juni na Julai.
"Hivi sasa hakuna mpunga mashambani ule wa mwanzo ulianza kuvunwa Mei na wengine wamevuna Juni, wakulima wengi hivi sasa wananunua mchele kwa wachuuzi," alisema Bw. Simchimba.
Akizungumzia hali hiyo Ofisa mtendaji wa Kata ya Kamsamba Bw. Emmanuel Msukwa alisema kuwa amekuta desturi hiyo kwa wakulima wa mpunga wa bonde la Kamsamba na kwamba hali hiyo imetokana na wakulima hao kutothamini ugumu wa kazi wanayoifanya na kupenda starehe ya muda mfupi isiyo na tija.
Alisema kuwa mkulima anasahau kuwa anatumia nguvu na gharama kubwa katika kuandaa shamba, kulitunza na kupalilia na kwamba inapofika wakati wa mavuno anajikuta akiishia kubadilishana mazao yake na pombe ambayo haimpi shibe wala manufaa kwa familia yake.
du ulevi noma!
ReplyDelete