Na Florah Temba, Moshi
KATIKA kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu, wakuu wa wilaya mkoani Kilimanjaro na majirani zao wa Kenya wamekubaliana kushirikiana kudhibiti njia zote wanazopitia na
kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaotumika kuwasafirisha.
Akizungumza katika kikao walichokaa wakuu hao wa wilaya mkoa wa Kilimanjaro na wakuu wilaya kutoka wilaya ya Taveta na Lotokitok nchini Kenya kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Bw. Peter Toima alisema wameazimia kuainisha njia zote wanazotumia wahamiaji haramu kuingia nchini ili kuwadhibiti wasiingie katika nchi hizo.
Bw. Toima alisema pamoja na kuainisha njia hizo pia wameazimia kuwatafuta watu ambao wanatumika kuwasafirisha wahamiaji hao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao kukomesha tabia hiyo.
"Tumejipanga kuimarisha ushirikiano katika kudhibiti wahamiaji haramu
wanaoingia nchini kinyemela, tumepanga kubainisha njia zote ambazo wanatumia na kuzidhibiti pamoja na kuwatafuta watu wanaotumika kuwasafirisha ili kuwachukulia hatua kali za kisheria," alisema Bw. Toima.
Aidha wakuu hao walisisitiza kuwa wahamiaji haramu wanapokamatwa na hatimaye kufikia hatua ya kurudishwa makwao utaratibu wa kuwarudisha uzingatie sheria badala ya kuwatelekeza maeneo ya mipakani.
Walivitaka vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Kilimanjaro na nchini Kenya kuendelea kushirikiana katika doria na kupeana taarifa mbalimbali za kiuhalifu pamoja na misako.
Polisi wapatiwe usafiri wa uhakika na mafuta ya kutosha ili kutekeleza kwa ufanisi kazi zao za kupambana na matukio ya kiuhalifu.
No comments:
Post a Comment