04 July 2011

Sita: Wawekezaji wa ndani walindwe

Na Grace Michael, Dodoma

WAZIRI wa Afrika Mashariki Bw. Samuel Sitta amewataka wabunge kuweka nguvu nyingi katika kutetea maslahi ya wawekezaji wa ndani kwa kuwa kila
wanachokifanya kinakuwa ni kwa faida ya nchi.

Bw. Sitta aliyasema hayo juzi usiku kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango maalumu wa kusomesha mtoto wa mkulima wa zabibu iliyofanyika katika viwanja vya Bunge mjini
Dodoma.

Mpango huo unatekelezwa na Kampuni ya Tanzania Distilleries Ltd, ambapo katika awamu hii imechukua watoto 10 wa wakulima wa zabibu ambao watasomeshwa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Kilichofanywa na TDL ni kikubwa mno na hapa ndipo tunaona umuhimu wa wawekezaji wa ndani…hivyo ndugu zangu wabunge ni vyema tukatetea zaidi wawekewzaji wa ndani ambao wanajua umuhimu wa nchi na wanachokifanya mwisho wake ni kwa maslahi ya nchi lakini wawekezaji wan je hasa wa madini hawafanyi haya,” alisema Bw. Sitta.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa TDL ili ifanikishe mpango wake hasa katika uwekezaji walioufanya katika sekta ya kilimo katika zao la zabibu.

Awali, Mkurugenzi wa TDL, Bw. David Mgwasa alisema kuwa pamoja na nia njema waliyonayo ya kushirikiana na wakulima wa zabibu, lakini juhudi zao zinakwamishwa na kodi kubwa iliyowekwa na serikali katika mvinyo unaotengenezwa na TDL.

Akizungumzia hilo, Bw. Sitta alisema kuwa suala hilo limewafikia wabunge kwa kuchelewa lakini akaahidi kuwa serikali inaweza ikaangalia namna ya kuwasaidia
zaidi ili waweze kufanikisha malengo yao.

"Nasikitika kuwa hili la kodi mmetuambia wakati tayari bajeti imeshapita na kodi hizo zimepitishwa…ni kweli mpango mlionao ni mzuri hasa wa kuwakumbuka hata
watoto wa wakulima wa zabibu lakini serikali inawajali na itaendelea na ushirikiano,” alisema Bw. Sitta.

Naye Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda aliwataka wabunge wa Mkoa wa Dodoma kuanzisha umoja wa wakulima wa zabibu ili kuwawezesha kufanya vizuri zaidi na hatimaye wakaona faida ya kilimo chao.

Mpango huo uanatarajiwa kusomesha watoto wasiopungua 500 katika elimu ya ngazi ya sekondari na kwa kuanzia jumla ya watoto 50 watachaguliwa katika kipindi kinachoanzia Julai mwaka huu na Januari 2012.

No comments:

Post a Comment