*Sheria ya mkopo kuwabana
Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ufafanuzi juu ya kanuni zinazotumika kuwatoa wachezaji kwa mkopo na kwamba, hakuna klabu
itakayoruhusiwa kutoa au kupokea wachezaji wanaozidi watano kwa mkopo.
Kwa mantiki hiyo, Klabu ya Simba ambayo imewatoa wachezaji 13 kwa mkopo kwenda klabu mbalimbali zitakazoshiriki Ligi Kuu Bara, italazimika kupunguza wanane ili iendane na kanuni hiyo.
Lakini, inaweza ikaepuka janga hilo kwa kuhakikisha inamalizia nafasi nne walizoziacha wazi kutokana na kuwasilisha majina 26 ya wachezaji waliowaombea usajili kwa ajili ya msimu ujao na kubakiwa na nne ambazo zitakidhi kanuni hiyo.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana baada ya kuulizwa swali kuhusu taratibu za usajili kwa wachezaji wanaotolewa kwa mkopo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kwa mujibu wa kanuni za TFF ibara ya 42(5) kinaeleza kwamba, hakuna klabu itakayotoa au kupokea wachezaji zaidi ya watano kwa mkopo.
"Unajua hili suala la kuhamisha wachezaji kwa mkopo linaonekana kwa klabu zetu za hapa nyumbani kama halijaeleweka na ndio maana kila msimu lazima kuwepo na utata katika suala hili," alisema Wambura na kuongeza;
"Kutokana na hali hiyo, kesho (leo) tutakuwa na mkutano maalumu kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo ambapo tutakuwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Haki na Hadhi kwa wachezaji pamoja na watu wengine ili kutoa somo katika hilo," alisema.
Alisema timu inapotoa mchezaji kwa mkopo ni lazima kuwepo makubaliano ya pande tatu, mchezaji mwenyewe, timu yake na timu anayokwenda kwa kuandikishiana kwa maandishi ndipo taratibu za uhamisho zinapokuwa zimekamilika.
Aliongeza kwamba, mwisho wa kuwasilisha pingamizi ni Julai 31, na kwamba kamati husika itakaa na kuzipitia pingamizi hizo kati ya Agosti 1 mpaka 5 na kwamba, suala la beki wa Yanga, Oscar Joshua litashughulikiwa wiki hii.
Wachezaji ambao Simba imewatoa kwa mkopo na timu wanazotakiwa kwenda kwenye mabani ni Juma Jabu, Salum Aziz na Haruna Shamte (Moro United), Ali Ahmed 'Shiboli' (Kagera Sygar), Meshack Abel (African Lyon), Athuman Idd 'Chuji' na Mohamed Kijuso (Villa Squad).
Wengine ni Aziz Gilla, Mbwana Bakari (Coastal Union), Paul Terry na Godfrey Wambura (Moro United).
Haya ni matatizo yanayosabishwa na viongozi wa timu wanao taka kujiusisha na mambo ya usajili wa wachezaji badala ya kocha.Hebu angalia tu kwa kifupi timu imeacha zaidi ya wachezaji 13 inamaana Simba sasa ina karibu ya wachezaji 18 ambao ni wapya.Je hawa wachezaji wanaweza kuzoeana katika muda mfupi?,Mambo yatakuwa kama yaleyale ya msimu uliopita kwenye mashindano makubwa kila wakitia mguu uwanjani wanatolewa.Ulishaona Manchester united,Arsenal,Barcelona au timu nyingine kubwa katika bara la ulaya zinasajili wachezaji 15 katika msimu mmoja?Sijui Simba na Yanga watajifunza lini katika mambo ya soka.
ReplyDelete