Na Humphrey Shao
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inatarajia kuamdaa hafla ya kuzipongeza timu za Simba na Yanga, kwa kufika hatua ya fainali katika michuano ya
Kagame Castle Cup, baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecksadick, alisema kuwa timu hizo ziliwakilisha nchi vizuri, hivyo zinastahili kupongezwa.
"Timu hizi zinatoka Mkoa wa Dar es Salaam, ambao ninaungoza, ofisi yangu imeona ni vema kuzipongeza ili iwe changamoto kwa nyingine," alisema.
Alisema zikicheza hatua za mwanzo, mashabiki wengi walizitabiria vibaya timu hizo, lakini zilifanya maajabu mpaka zikafanikiwa kukutana katika mechi ya fainali.
Kaimu Mkuu wa mkoa huyo, alisema pamoja na Yanga kutwaa ubingwa, lakini pia Simba ni bora tofauti na wadau wa soka wanavyosema.
“Ni lazima tukubali, timu mbili zinapokutana, lazima moja ifungwe, hasa katika mechi ya fainali,” alisema.
Alitoa wito kwa timu hizo kuacha malumbano na badala yake, waanze kuzijenga upya timu zao kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment