28 July 2011

Pele Balozi wa Kombe la Dunia 2014

BRASILIA, Brazil

MCHEZAJI wa zamani wa soka Pele amekubali mwaliko wa Rais wa Brazil, Dilma Rousseff kuwa Balozi wa fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kufanyika nchini humo
mwaka 2014.

Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), liliripoti jana kuwa, mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 70, alisema ni heshima kubwa kupewa wadhifa huo, hivyo hawezi kukataa.

"Tangu fainali za kwanza za Kombe la Dunia nilizocheza mwaka 1958, nilikuwa nikifanya kazi kama hiyo, niliitetea na kuitangaza Brazil. Ni jukumu kubwa na siwezi kukataa mwaliko huo," alisema Pele.

Pele aliwaambia raia wenzake kujivunia kuandaa michuano hiyo  na kuweka kando shutuma za kucheleweshwa maandalizi ya fainali hizo kubwa bora.

Waziri wa Michezo wa nchi hiyo,  Orlando Silva, alisema Pele ni chaguo halisi kutokana na kazi aliyoifanya katika medani ya soka nchini humo.

"Ni mtu ambaye anafahamu mengi kwenye  ulimwengu wa soka, atatusaidia na kutuwakilisha,' alisema waziri huyo.

Pele amewahi kutwaa taji la Kombe la Dunia mara tatu kati ya mwaka 1958, 1962 na 1970 na mara zote ndiye amekuwa mfungaji bora, baada ya kuzifumania nyavu mara 1,281.

No comments:

Post a Comment