28 July 2011

Mbwana kuzichapa na Miyeyusho Jumamosi

Na Mwali Ibrahim

BONDIA wa ngumi za kulipwa, Mbwana Matumla anatarajia kutetea mkanda wake wa ubingwa wa UBO dhidi ya Farancis Miyeyusho katika pambano litakalofanyika
Julai 30, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Pambano hilo la uzito wa bantum raundi 10, litakuwa la upinzani kutokana na viwango vya mabondia hao kuwa vizuri.

Mbali na pambano hilo, litatanguliwa na pambano la marudiano kati ya Juma Fundi na Fadhili Majia anayetetea mkanda wake wa Shirikisho la Masumbwi Tanzania (PST).

Fadhili na Juma wanarudiana baada ya kutoka sare katika pambano la ubingwa huo lililofanyika hivi karibuni, litakuwa la uzito wa bantum.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Darworld Length Limited, Mohamed Bawaziri, ambaye ndiye mratibu wa mapambano hayo, alisema maandalizi ya mapambano hayo yanaendelea vizuri.

Mapambano mengine ya utangulizi ni kati ya Mkenya Gabriel Ocheng na Nasibu Ramadhani, pambano litakalokuwa la raundi 10.

Alisema kutakuwa na pambano la mabondia wanawake, ambalo litakuwa la kuhamasisha.

Mabondia wengine watakaopanda ulingoni kabla ya pambano kubwa  ni kati ya Mohamed Matumla na Ramadhani Mashudu, Ramdhani Shauri na Issa Shewe, huku Paul Samwel akizichapa na Hassan Kidobe.

No comments:

Post a Comment