Na Nyakasagani Masenza
WAZIRI Mkuu wa zamani, Bw. Edward Lowassa jana alikuwa miongoni mwa mamia ya watu waliofika nyumbani kwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Marehemu
Danny Mwakiteleko aliyefariki dunia juzi na kusema kuwa waandishi wa habari nchini wamepoteza kiungo mahimu katika tasnia ya habari nchini.
Bw. Lowassa aliyeongozana na mkewe, Regina Lowassa, alisema Bw. Mwakiteleko ni taa yenye mwanga iliyozimika ghafla.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nyumbani kwa Marehemu, Tabata Chang'ombe, Dar es Salam jana, Bw. Lowassa alisema Marehemu Mwakiteleko alikuwa mwandishi makini aliyefanya kazi yake kwa ajili ya maslahi ya Taifa.
Alisema wahariri, jamii na Taifa kwa ujumla wamepoteza mwandishi mahili aliyesimama imara kutetea jamii kupitia kalamu yake.
"Mimi binafsi na familia yangu, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Monduli, tunaipa familia yake pole nyingi. Naomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja ya kweli hasa katika kipindi hiki cha majonzi," alisema.
Aliwataka waandishi wa habari nchini kuiga mfano wa uandishi wa marehemu Mwakiteleko.
Kibanda kuwakilisha wahariri
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanazania (TEF), Bw. Absalom Kibanda atawakilisha wahariri wenzake katika msafara wa mazishi ya Marehemu Mwakiteleko mkoani Mbeya.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa TEF, Bw. Neville Meena ilisema kuwa katika msafara huo, Bw. Kibanda ataambatana na mwakilishi wa jukwaa hilo kutoka Zanzibar ambaye jina lake halikutajwa.
Bw. Mwakiteleko alifariki dunia saa 10 alfajiri, Jumamosi Julai 23, 2011 kufuatia majeraha aliyoyapata kichwani kwenye ajali ya gari Julai 20, 2011 katika eneo la Tabata TIOT saa nne usiku alipokuwa akirejea kutoka kazini.
Mauti yalikuta Danny zikiwa zimepita siku sita, tangu wahariri waliporejea kutoka mkoani Arusha na Kilimanjaro, ambako walikutana kujadili mustakabali wa taaluma ya habari nchini, yeye akiwa miongoni mwa wahariri 80 waliohudhuria, wakiwa na mada kuu isemayo "Uandishi wa Habari unaozingatia wajibu".
"Wahariri wengi tunakumbuka michango yake muhimu katika mkutano ule ambayo tunaweza kuuita 'Wosia wake wa mwisho kwa wahariri wenzake'. Kwa hakika Jukwaa la Wahariri limepoteza mwanachama wake mahiri," ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:
"Danny ametutoka katika kipindi ambacho Jukwaa tulikuwa bado tunahitaji mchango wake kuimarisha jukwaa letu. Lakini zaidi ni katika chumba cha habari cha New Habari Ltd, ambako tunaamini kwamba wamepoteza mwanahabri na mhariri.
Danny atakumbukwa pia kwa mchango mkubwa aliyoutoa katika mageuzi ya mfumo wa sekta ya habari nchini. Vyumba vya habari vya magazeti ya Majira, Mwananchi na hata New Habari Ltd, ni mashahidi wa mchango wake. Mwanzoni mwa miaka ya 90, Danny alikuwa mmoja wa wanahabari walioshiriki kuiingiza habari katika sekta binafsi, akiwa mmoja wa wahariri viongozi katika vyumba vya habari.
Tumempoteza mpiganaji mwingine Danny Mwakiteleko. kwa wale waliokuwa UDSM miaka ya tisini wakati wa together we stand alikuwa mstari wa mbele kwenye hilo na alishiriki mgomo ule kwa asilimia mia moja. vile vile wale watoto wa nusu mungu pale JKT mafinga hasa Danger coy tumepoteza mpiganaji. MUNGU AILAZE PEPONI ROHO YA MAREHEMU DANNY. RAHA YA MILELE UMPE BWANA APUMZIKE KWA AMANI. TOGETHER WE STAND DANNY BYE!
ReplyDelete