Na Mary Margwe, Simanjiro
WAJUMBE wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mererani mkoani Manyara wamepinga kitendo cha Halmashauri ya Wilaya hiyo kuandaa uchaguzi mdogo kwenye vitongoji viwili vya
mji huo badala ya vitatu kwani wamekiuka agizo la serikali la kutambua vitongoji hivyo.
Wakizungumza jana kwenye kikao cha mamlaka hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mamlaka hiyo, wajumbe hao walidai kuwa uchaguzi mdogo unatakiwa kufanyika kwenye vitongoji vyote vitatu na siyo viwili kama ilivyopendekezwa.
Walidai kuwa tangazo la Gazeti la Serikali, liliagiza kugawa kitongoji cha Kazamoyo kuwa vitongoji vitatu, baada ya kuanzishwa vitongoji vipya vya Kazamoyo juu na Mji mpya, hivyo uchaguzi ufanyike kwenye vitongoji vyote.
Mmoja kati ya wajumbe hao, Bi. Kaanaeli Minja alisema kutokana na mgawanyiko huo, vitongoji vyote vitatu vinatakiwa kufanya uchaguzi upya kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo, naye kugombea na siyo vitongoji vipya vya Kazamoyo juu na Mji mpya.
Huko ni kukiuka utaratibu na kubebana, inatakiwa vitongoji vyote vitatu vifanye uchaguzi pamoja na Kazamoyo, kwani watu waliompa kura Mwenyekiti wa sasa wamehamia mitaa mipya hivyo naye agombee upya," alisema Bi. Minja.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Zaire kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Said Kuzecha alidai kuwa anashangazwa na watendaji wa mji huo waliopata barua ya maelezo ya uchaguzi huo, Julai 4, mwaka huu, na kuwajulisha Julai 19, mwaka huu.
"Watendaji na nyie hivi sasa mmekuwa wanasiasa jamani kwa nini mkalie barua za uchaguzi ili hali zinaonyesha baada ya siku 60 uchaguzi ufanyike, inaonesha mnataka kuhujumu na kutuletea kabla ya siku nne ili tushindwe," alisema Bw. Kuzecha.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa mji huo, Bw. Nelson Msangi alisema wameona mapungufu kwenye maelezo ya utaratibu wa kufanyika uchaguzi huo mdogo hivyo ataandika barua ili apate muongozo kamili kutoka ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment