Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wa Yanga, Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza na Davies Mwape, wanauumiza kichwa uongozi wa timu hiyo kwa kushindwa kurudi kwa wakati, huku timu hiyo
ikiwapa muda mpaka leo wawe wameripoti kambini.
Wachezaji hao waliahidi kurudi kabla ya timu hiyo kwenda bungeni kuwaonesha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Kombe la Kagame walilotwaa Julai 10, mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Selestine Mwesigwa, alisema baada ya kutoka bungeni, wachezaji waliruhusiwa kwenda nyumbani kwao, lakini leo wanaendelea na mazoezi kama kawaida.
"Kuhusu wachezaji wa kigeni (Kiiza, Niyonzima na Mwape), ambao hawakufika, tunatarajia kesho (leo) watakuwepo katika mazoezi kwani tumeshawasiliana nao, hivyo watakuja tu," alisema Mwesiga.
Akizungumzia michezo mingine ya kirafiki baada ya kufungwa mabao 2-1 na Polisi Dodoma, alisema hiyo ipo katika programu za Kocha Sam Timbe ambaye alitarajiwa kurudi jana jioni.
Alisema atakaporudi watakaa na Msaidizi wake, Fred Felix Minziro, kuangalia waanze na programu ipi ambapo kama kutahitajika mechi za kirafiki, watatoa taarifa kwa uongozi.
Pia, alizungumzia hatima ya beki wao mpya, Oscar Joshua, alisema suala hilo lipo mikononi mwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wao ndio watakaojua mchezaji huyo aichezee timu ipi msimu ujao.
Naye, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, kabla ya Mwesigwa kuzungumzia suala la akina Kiiza, alisema wachezaji hao wamewapa muda mpaka leo wawe wameripoti kambini, wasiporipoti watajua jinsi gani ya kushughulika nao.
Alisema ni vizuri wachezaji wote wakaripoti kambini kwa wakati ili wakipewa mbinu za kiufundi wapewe kwa pamoja kuliko kufanya mazoezi na wachache.
No comments:
Post a Comment