26 July 2011

Mbunge aikejeli CCM kushindwa umaskini

Na godfrey Ismaely, Dodoma

MBUNGE wa Kilwa Kusini, Bw. Selemani Bungara (CUF), ameikejeli Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiishukuru kwa kushindwa kuondoa maadui wa
maendeleo katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru.

Akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, mbunge huyo alisema wakati taifa linaelekea kusherehekea miaka 50 ya uhuru bado, CCM imeshindwa kuondoa ujinga, maradhi na umaskini hali inayowafanya wananchi kuelemewa na mizigo.

“Miaka 50 ya Uhuru bado hatujaweza kujitegemea, Mwalimu Nyerere alisema asiyeweza kujitegemea hayupo huru, mpaka sasa asilimia 87 ya bajeti hii tunategemea wafadhili, tunaishukuru serikali ya CCM kwa kutufikisha hapa tukiwapa miaka mingine 50 watatufikisha kubaya zaidi,” alisema Bw. Bugara.

Akizungumzia juu ya wakulima wa ufuta Kilwa, mbunge huyo alisema viongozi wa serikali mkoani humo wamekuwa wakiwazuia kuuza zao hilo kwa bei nzuri na kuwapongeza viongozi hao kwa kuwapa nguvu wapinzani.

“Sisi watu wa Kilwa tunaonewa sana, wakulima wanapanda wenyewe, wanapalilia wenyewe, lakini wakianza kuvuna serikali inakuja na kuwataka kuuza kwenye vyama vya ushirika ambako ni sh 1,000 kwa kilo na kuwakataza kuuza kwingine ambako ni sh 1,500,” alisema mbunge huyo.

“Hayo ndio matunda ya CCM. Nilimwandikia barua Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya kuwa wakulima wa Kilwa wanaonewa, sijajibiwa mpaka leo.

“Kuna kikundi kidogo cha watu kinaongozwa na Mkuu wa Mkoa kuwanyonya wakulima wa ufuta. Haiwezekani awazuie kuuza kwenye bei nzuri. Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo wanamuogopa Mkuu wa Mkoa,” alisema na kuongeza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa  yupo 'chubwachubwa', mara Lindi mara Dar es Salaam hivyo
haieleweki," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema hatawashinikiza wakulima hao kuandamana, kwani bila kufanya hivyo serikali haitawasikiliza.


Pamoja na hayo, alimtaka Profesa Maghembe kutoa tamko kwamba wakulima hao wauze ufuta katika chama  chochote.

“Katika hili nitatoa shilingi, ingawa najua sitafanikiwa kwa kuwa wabunge wa CCM ni wengi. Nikishindwa nitaandamana usiku na mchana. Nataka wakulima wa ufuta wawe huru,” alisema na kuongeza kuwa chama legelege huzaa serikali legelege.

Kwa upande wake, mbunge wa Geita, Donald Max (CCM), alieleza kushangazwa na aliyebuni trekta ndogo ziiitwazo Power Tiller na kuongeza kuwa haziwanufaishi wakulima walio wengi.

“Power Tiller watu wanazolea mawe na matofali, kabla hatujafanya kitu tufanyeni utafiti, kwani haziwasaidii wakulima,” alisema mbunge huyo.

2 comments:

  1. Bwana Bungara tetea wakulima hao wengine wameshiba kwa sasa kwa hivyo wamesahau walikotoka.

    Kuhusu power tillers hazina ubaya wo wote pindi zikitumika pale zilipokuwa designed kwa kazi hiyo, mfano kwenye mabonde ya mpunga ambapo udongo wake uko laini.

    Huwezi kutumia power tiller kwenye udongo wa mfinyanzi kama ule wa Mwanza hapo utakuwa umeula mkavu.

    ReplyDelete
  2. bwana bungara usitusahahu na sisi wakulima wakorosho wa mtwara maana wabunge wetu wa CCM wamelala usingizi mzito mkubwa bungeni. naomba ututee wakulima wa korosho mtwara kwa maana serikali haijui gharama tunazoingia kwa ajili ya kuzalisha korosho, leo hii wakati unauza ndio wanakuja wanataka kukupangia bei ya kuuzia huu ni uhuni, udharirishaji kwani tulipodai uhuru kutoka kwa wakoloni tulikuwa tunataka kuwa na uhuru si wa nchi bali kwa mtu mmoja mmoja tu kuamua mambo yako ikiwemo nani utamuuzia bidhaa na kwa kiasi gani gani na siyo serikali ikupangie umuuzie nani kwa kiasi gani huku ni kupora uhuru wa mtu binafsi kujiamulia mambo yake mwenyewe.

    ReplyDelete