Na Peter Mwenda
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Emmanuel Nchimbi ameongoza maelfu ya waombolezaji kuaga mwili wa Naibu Mhariri Mtendaji wa
New Habari 2006 Ltd, Danny Mwakiteleko kabla ya kusafirishwa kuzikwa nyumbani kwao Tukuyu, Mbeya.
Bw. Nchimbi akitoa salamu za wizara yake alisema amefarijika kuona ushirikiano na mshikamano wa wanahabari tangu ajali ilipotokea, hospitalini na baada ya kifo cha Mwakiteleko.
Alisema katika misiba yote aliyowahi kuhudhuria ya wanahabari, hajawahi kuona waajiri wakiahidi kusaidia familia ya marehemu lakini New Habari wanapaswa kuigwa na vyombo vingine.
Katika salamu za rambirambi, Kampuni ya New Habari 2006 Ltd imeahidi kumlipa mke wa marehemu Mwakiteleko mshahara ya kila mwezi kwa miaka mitano, kusomesha watoto wake wawili na watoto wa marehemu kaka yake hadi Chuo Kikuu.
Mtendaji Mkuu wa New habari 2006 Ltd, Bw. Hussein Bashe alisema mtoto wa kwanza wa marehemu Mwakiteleko anayesoma kitado cha tatu na mdogo wake anayesoma darasa la sita watapewa heshima kama baba yao alivyofanya kazi kwa uadilifu katika kampuni hiyo.
Bw. Bashe alisema Mwenyekiti Mtendaji wa New Habari 2006 Ltd, Bw. Rostam Aziz ameahidi kuiangalia familia hiyo kwa karibu ikiwemo kuwasomesha watoto wawili wa kaka yake Mwakiteleko aliokuwa akiishi nao hadi elimu ya chuo kikuu.
Alisema marehemu Mwakiteleko alikuwa msikivu, mwajibikaji na mchapa kazi na kabla ya kifo chake alikuwa akiandaa toleo maalumu la miaka 50 ya Uhuru.
Jukwaa la wahariri katika salamu zao zilizosomwa na Bw. Manyerere Jackton zilisema marehemu ameacha funzo kubwa kwa wanahabari kujituma kwani kwa namna ya pekee anastahili kupata waombolezaji wengi kama walivyokuwa jana kutokana na tabia yake ya kupenda kazi.
Katika salamu mbalimbali zilizotolewa Waziri Nchimbi aliyemwakilisha Rais Kikwete alisema amesikitishwa na kifo hicho na kuahidi Ikulu kutoa mkono wa pole kwa familia hiyo.
Wengine waliotoa rambirambi zao ni Jukwaa la Wahiriri sh. 3,320,000, CRDB sh. mil. 1, NHC sh. 700,000, PPF sh. 500,000, Jeshi la Polisi Tanzania sh. 200,000 Kamati ya Nishati na Madini sh. 500,000 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe alitoa sh. 200,000 na Sport FM ya Dodoma sh. 100,000 na TANESCO sh. 500,000.
Wakati huo huo Chama cha Waandishi wa Habari wanawake (TAMWA) kimemwelezea marehemu Mwakiteleko kuwa alitumia nafasi yake kuchapisha habari bila ubaguzi wa kijinsia.
Alisema TAMWA itaendelea kumkumbuka marehemu Mwakitelekeo kutokana na moyo aliokuwa nao wa kushirikiana na watetezi wa haki za binadamu katika harakati za kukomesha ndoa za utotoni na mimba za mashuleni ambazo zinakwamisha watoto wa kike kupata elimu.
Marehemu Mwakiteleko alipata ajali Jumatato iliyopita saa 4:00 usiku katika eneo la TIOT, Tabata baada ya kukonga lori kwa nyuma wakati akitokea kazini kwenda nyumbani kwake Tabata Chang'ombe, na kufanyiwa upasuaji wa kichwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambao mauti yalimkuta Jumamosi alfariki.
Mwili wa marehemu Mwakiteleko ulisafirishwa jana kwenda Mwakaleli Tukuyu, Mbeya ambako anatarajiwa kuzikwa leo. Marehemu ameacha mke na watoto wawili. Mungu ilaze roho ya yake mahali pema peponi, Amen.
No comments:
Post a Comment