26 July 2011

Bajeti ndogo ya kilimo yakera Kamati, Upinzani

Na Godfrey Ismaely, Dodoma

KAMATI ya Bunge kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maji  imeitaka serikali kuchukua maamuzi magumu katika kuiwezesha Bajeti ya Wizara hiyo ili kuchangia
kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo mara baada ya bajeti ya wizara hiyo kuwasilishwa na Waziri Profesa Jumanne Maghembe  bungeni Dodoma jana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maji,  Profesa David Mwakyusa alisema kuwa sababu zinazochangia sekta ya kilimo nchini kushindwa kuongeza na kukuza uchumi wa taifa ni pamoja na bajeti finyu.

“Bajeti ya Wizara hii bado ni ndogo na hii ni sababu kubwa ya sekta hii kushindwa kuchangia kwa kiasi cha kutosha katika kukua kwa uchumi, hivyo kamati inatoa ushauri kwa serikali kuangalia njia za kuongeza bajeti na ikiwezekana kuchukua maamuzi mazito,” alisema Profesa Mwakiyusa.

Alisema licha ya zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania kujishughulisha na kilimo katika mwaka wa fedha 2009/10 sekta hiyo ilichangia asilimia 26 tu ya pato la taifa huku ukuaji wa kilimo ukiwa unashuka mwaka hadi mwaka.

“Katika mwaka 2008/09 kilimo kilikuwa kwa asilimia 4.2 tu, wakati huo huo idadi ya watu inakua kwa asilimia 2.9 wakati bajeti inayotengwa kwa kilimo imekuwa ikiongezeka kwa kiasi kidogo sana; alisema na kuongeza:

“Mwaka 2008/09 bajeti ilikuwa ni sh. bilioni 440 sawa na asilimia 6.4, mwaka 2009/10 sh. bilioni 666.9 sawa na asilimia saba, mwaka 2010,2011 sh. 903 bilioni sawa na asilimia 7.7 na mwaka 2011/12 sh. bilioni 926 sawa na
asilimia 6.7 tu ya bajeti ya serikali,” alisema Profesa Mwakiyusa.

Alisema ili bajeti hiyo iweze kuzisaidia sekta za kilimo serikali inapaswa kufikia kiwango kilichokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC cha asilimia 10 ya bajeti ya serikali ili kilimo kiweze kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.

Wakati huo huo Kambi ya Upinzani Bungeni ilieleza kusikitishwa na bajeti ndogo iliyotengwa kwa wizara hiyo kwa madai kuwa ilipaswa kupewa nguvu kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo, Msemaji wa kambi hiyo katika wizara hiyo, Bw. Meshack Opulukwa alisema kuwa hali hiyo inasikitisha zaidi kutokana na kiasi cha fedha za maendeleo kuwa kidogo ikilinganishwa na matumizi ya kawaida.

“Kambi ya upinzani inasikitishwa sana na bajeti iliyotengwa kidogo kwa wizara hii muhimu katika uchumi wetu, wizara ambayo inaongoza kwa kuajiri watu wengi yaani zaidi ya asilimia 70, sekta tunayotegemea kuinua sekta zingine kama viwanda,” alisema Bw. Opulukwa.

“Alisema kambi hiyo inasikitika zaidi kuona bajeti ya maendeleo inategemea zaidi fedha za nje kwa sababu katika kila sh. 100 itakayotumika kwa maendeleo, fedha ya ndani ni sh. 3.5. Bila kufanya nyongeza na maboresho katika wizara hii tutegemee upungufu wa chakula kuzidi kuongezeka zaidi kuliko ilivyo sasa,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment