13 June 2011

Mareklani kusaidia lishe ya watoto

Na Grace Michael

SERIKALI ya Marekani imeahidi kuongeza bajeti yake katika lishe kwa mtoto ndani ya siku 1,000 bajeti itakayofikia kiasi cha dola za Marekani milioni 6.7.Hayo
yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bi. Hilary Clinton wakati alipokutana na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri.

"Suala la lishe kwa mtoto tangu siku ya kwanza hadi siku ya 1,000 ni lazima litiliwe mkazo kwa kuwa lina umuhimu wa kipekee na kwa kutambua hilo, Marekani itaongeza bajeti yake mara nne ili kufikia kiasi cha dola milioni 6.7," alisema Bi. Clinton.

Alisema kuwa awali suala hilo halikuwekewa mkazo wa kipekee kutokana na kuwepo kwa vikwazo kati ya Sekta Binafsi, asasi zisizo za kiserikali pamoja na serikali kwa kuwa kila upande haukuelewa unatakiwa kufanya nini.

Alisema kuwa Marekani kwa kushirikiana na watu mbalimbali wamekuja na mtazamo mwingine kuhusu lishe ambao umeungwa mkono na ushahidi wa kisayansi ambao unaonesha kuwa kupatikana kwa lishe bora hasa kwa mtoto katika umri huo husaidia katika ukomavu wa kiakili kwa mtoto, hatua inayomfanya kuwa na tija kwa taifa katika siku za usoni.

"Suala hili linahitaji pia nguvu ya pamoja katika kulifanikisha, hivyo ni lazima kuwe na ushirikiano wa kutosha kati ya serikali na sekta binafsi lakini pia elimu kuhusu lishe inatakiwa kuwepo katika pande zote za nchi," alisema Bi. Clinton.

Kwa upande wa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alielezea namna serikali ilivyojipanga katika kukabiliana na suala la lishe nchini hasa katika siku 1,000 za mtoto.

Alisema kuwa serikali inaunga mkono suala hilo kwa kuwa ni moja ya mambo yaliyoko kwenye mpango wa milenia hivyo akasisitiza kuwa serikali iko tayari kufanikisha suala hilo.

Naye Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe alisema kuwa kuna mpango wa kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekari 334,000 hadi milioni moja ndani ya miaka 10 ili kuhakikisha tatizo la chakula linamalizika.

Bi. Clinton aliingia nchini juzi na leo anatarajia kukutana na Rais Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment