13 June 2011

Ole Millya chini ya uangalizi Arusha

Na Said Njuki Arusha

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha imeyatupilia mbali mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Siasa ya chama hicho
mkoa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa huo, Bw. James Millya na wenzake wafukuzwe uwanachama badala yake watuhumiwa hao wamepewa onyo, onyo kali na kuwekwa katika uangalizi maalumu kwa muda kati ya miezi sita na 12.

Hali hiyo imetokea baada ya mvutano wa muda mrefu baina ya Katibu wa CCM Mkoa, Bi. Mary Chatanda na vijana hao waliodaiwa kufanya maandamano wakishinikiza katibu huyo kuachia ngazi kwa madai ya kuachia majimbo mawili ya Karatu na Arusha mjini kuchukuliwa na wapinzani huku kata kadhaa pia zikieenda kwa wapinzani.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa usiku juzi baada ya kikao hicho na katibu wa mkoa, imeeleza kuwa Halmashauri hiyo iliyoketi juzi kwa takribani saa saba, imebadilisha adhabu iliyokuwa imependekezwa na kamati hizo za Usalama na Maadili na Kamati ya Siasa ya Mkoa ya kuwavua uwanachama wa CCM na kuamua kutoa onyo na onyo kali kwa wadaiwa hao.

Waliopewa onyo kali kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili toleo la februari 2010 ibara ya 8 (2) (ii) (b) na kuwepo katika uchunguzi wa mienendo yao ndani ya chama kwa muda wa miezi 12 ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa, Bw. Millya, mjumbe wa baraza kuu la umoja huo, Bw. Mrisho Gambo na wanachama wa chama hicho ambao ni Bw. John Nyiti, Bw. Ally Bananga na Bw. Ally Majeshi.

Waliopewa adhabu ya onyo na kuwa katika uangalizi wa muda wa miezi sita, ni wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya mkoa, makatibu wa umoja huo wa wilaya ambao ni Ezekiel Mollel (Monduli) na Ally Rajabu toka Karatu, huku wanachama wengine wa umoja huo wa vijana, Fatuma Ngairo (Arusha), Filomen Ammo (Arusha) na Preygod Kivuyo (Monduli).

Sanjari na hilo Halmashauri hiyo imefuta hoja iliyodaiwa kujengeka katika mgogoro huo ya kumtaka katibu Chatanda aondoke mkoani hapa kwa kile kilichodaiwa ni kufanya kazi kibabe na kutokuwajibika ipasavyo hatua hali iliyodaiwa kuwa ndiyo sababu ya kushindwa kwa chama hicho.

Hata hivyo Halmashauri hiyo imemtaka Bw. Millya kumwomba radhi katibu Chatanda kwa madai ya kutoa kauli za matusi, kashfa na lugha za uzalilishaji dhidi ya katibu huyo, huku ikimtaka mjumbe wa baraza la vijana, Bw. Gambo kumpigia goti aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Arusha Mjini, Dkt.  Batilda Burian kwa kauli zake za matusi, kashfa na udhalilishaji wa kijinsia.

Pia kikao hicho, kimelaani vikali vitendo vya vijana kufanya maandamano ya Mei 19, mwaka huu na kuagiza kwa msisitizo kwamba mtindo huo ukome na usirudiwe tena na kwenda mbali zaidi na kueleza kuwa hoja na malalamiko yote yafuate taratibu za vikao ndani ya chama na si vinginevyo.

2 comments:

  1. Ukweli kabisa Mary Chatanda ni mbabe sana lakini pia amewekwa na wakubwa zake (CCM) kwa maslahi yao binafsi. Sasa nani wa kumwondoa mtaandamana sana vijana mtatukana sana nani anayewasikia? Msipoteza nguvu zenu buuure mama huyo ni wa wenyewe jamani. Nyie mlie tu Chatanda mashine kubwa hiyo. Na huyo ndiye anaua CCM Arusha wala si uongo lakini nani wa kumfunga paka kengele?

    ReplyDelete
  2. MLICHOKIFANYA SIYO KUTATUA TATIZO BALI NI KUFUNIKA KIKOMBE MWANAHARAMU APITE. FUNIKA MAOVU KWA AJILI YA MSHIKAMANO LAKINI MKUMBUKE KWAMBA WASWAHLI WALISEMA MFICHA MARADHI MAUTI ITAMUUMBUA.

    ReplyDelete